*YALIYOJIRI LEO FEBRUARI 17, 2020 WAKATI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AKIZINDUA KIPINDI CHA PILI CHA AWAMU YA TATU YA MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII TASAF*
*Aliyoyasema Rais Dkt. Magufuli*
#Kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika, hali ya umaskini nchini inazidi kupungua. Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti ya Benki ya Dunia ya Septemba, 2019 imeitaja Tanzania kuongoza kwa kasi ya kupambana na umaskini kati ya nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa jangwa la Sahara.
#Nawapongeza viongozi wote waliohusika katika kutekeleza mpango huu, watendaji wa Serikali zote mbili pamoja na wafadhili wote tunaoshirikiana nao kwani matokeo ya mpango huo yameweza kupunguza umaskini katika jamii.
#Kupitia zoezi la uhakiki wa Kaya maskini lililofanyika Novemba 2015 hadi Juni, 2017 limebaini uwepo wa Kaya hewa 73,561, hii ni changamoto kubwa,Naagiza tatizo hili lidhibitiwe.
#Jumla ya 67% ya kiasi cha fedha kilikua kikielekezwa kwenye kutoa ruzuku, awamu hii ambayo itatumia sh.Trilioni 2.032 tumeboresha kwa kupunguza kiasi cha ruzuku kufikia 38% na 60% ya fedha hizo ambayo ni sawa na sh. Trilioni 1.22 itatumika kwenye miradi ya maendeleo.
#Awamu hii itatekelezwa katika Halmashauri 185 za Tanzania Bara na Wilaya 11 za Zanzibar. Miradi itakayotekelezwa itahusu sekta za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na mazingira, Pia kupitia miradi hiyo tunatarajia kuzalisha ajira kwa watu Mil.1.2
#Natoa wito kwa wahusika wote kusimamia vizuri mradi huu kwani licha ya nchi na taasisi nyingi kutufadhili, fedha nyingi ni za mkopo hivyo muhakikishe mnasimamia vizuri mradi huu ili malengo ya kukopa fedha hizo yaweze kutimia.
*Waliyoyasema viongozi wengine*
#Natoa rai kwa wanaohusika na Mpango huu kuendelea kuwa na weledi katika kusimamia mpango huu ili kuendelea kupata matokeo bora kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita - Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
#Napenda kuwakumbusha Watanzania kuwa TASAF ni mradi wa Serikali, unagharamiwa kwa kutenga fedha katika bajeti za kila mwaka pamoja na kukopa fedha ambazo pia zitalipwa na Serikali hivyo zitumike kwa usahihi - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika.
#Awamu ya tatu ya TASAF kwa upande wa Zanzibar hadi kufikia Oktoba, 2019 imetumia zaidi ya shilingi Bilioni 4.6 kwa shughuli mbalimbali - Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed.
#Tunajivunia sana kuona maendeleo ya mpango huu wa TASAF yaliyopatikana kwa miaka iliyopita, hasa katika kuwainua wanawake nchini - Muwakilishi kutoka Benki ya Dunia, Preeti Arora.
#Naipongeza nchi ya Tanzania kwa hatua hii ya kuendeleza mradi huu muhimu unaonyanyua maisha ya watanzania pamoja na kupunguza umaskini nchini - Balozi wa Sweeden, Anders Sjoberg.
#Kupungua kwa umaskini ni hali inayoenda hatua kwa hatua, kasi ya kupungua kwa umaskini nchini inaenda kwa mwendo kasi ambapo hali ya umaskini wa kipato umetoka 34% mwaka 2007, 28.4% mwaka 2012 na kufikia 26.4% kwa mwaka 2018 - Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka (NBS)Dkt. Albina Chuwa.
#TASAF imechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza umaskini,kwa mwaka 2018 kupitia mpango huo umaskini umepungua kwa 0.2%, ni asilimia kubwa sana - Mkurugenzi NBS, Dkt. Albina Chuwa.
#TASAF ya Awamu ya Tatu ilianza rasmi Februari, 2013 na unatarajia kumalizika mwaka 2023 ambapo kipindi cha kwanza kimekamilika na leo kinazinduliwa kipindi cha pili - Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga.
#Kipindi cha kwanza cha awamu hii ya tatu jumla ya shilingi Trilioni 1.46 zimetumika ambapo utekelezaji wake umefanyika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 159 na katika Serikali ya Zanzibar utekelezaji umefanyika katika wilaya zote - Ladislaus Mwamanga.
#Utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Awamu ya Tatu umeleta manufaa makubwa kwani zaidi ya Kaya maskini Mil.1.1 zenye jumla ya watu 5,296,470 zilipatiwa ruzuku - Ladislaus Mwamanga.
#Wanafunzi zaidi ya Milioni 1.8 waliandikishwa katika Shule za Msingi, wanafunzi 448,409 Shule za Sekondari na wanafunzi 277 waliomaliza kidato cha 6 walipata mikopo ya kujiunga na Vyuo Vikuu nchini - Ladislaus Mwamanga.
#Jumla ya Kaya 253,117 zilishiriki katika miradi inayotoa ajira za muda, miradi 8809 yenye thamani ya sh. Bilioni 130 iliibuliwa na kutekelezwa na jamii - Ladislaus Mwamanga.
#TASAF ya Awamu iliyopita imewanufaisha sana wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo jumla ya mitaa 304 kati ya mitaa 564 imenufaika na fedha zitolewazo na mpango huo - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.