Wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Arusha, wilayani Arumeru, wametakiwa kunawa mikono kwa kuzingatia kanuni na hatua sahihi za unawaji mikono, kwa kutumia maji safi na sabuni ili kujikinga na magonjwa yatokanayo na uchafu wa mikono.
Rai hiyo imetolewa na mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya Kunawa Mikono Duniani, Afisa Usafishaji na Mazingira, halmashauri ya Arusha, Vanika Ndelemu, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, yaliyofanyika kwenye viwanja vya kanisa la KKT Usharika wa Ilkiding'a.
Afisa Usafishaji huyo, amesema kuwa, endapo wananchi watazingatia kanuni sahihi za unawaji mikono, wataondokana na magonjwa, yanayotokana na uchafu wa mikono na kufanya bajeti ya dawa inayotumika kutibu magonjwa hayo, kuweza kutumika kutatua changamoto nyingine zinazowakabili wananchi.
Ameongeza kuwa, magonjwa yanayotokana na uchafu wa mikono, yanaepukika na hayapaswi kuwepo katika familia na jamii zetu, hivyo ni vyema kujipanga kuyapiga vita kwa kuchukua tahadhari binafsi kwa kunawa mikono kwa kutumia maji safi na sabuni.
" Kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 861.2 kwaajili ya kununulia dawa na vifaa tiba, endapo tutajikinga na magonjwa yatokanayo na mikono michafu, sehemu ya fedha hizo iingetumika, kuimarisha miundo mbinu ya barabara na maji pamoja na shughuli nyingine" amefafanua Mgeni rasmi huyo.
Aidha, amewaagiza Maafisa watendaji wa kata na vijiji kusimamia, uundaji wa Kamati za ufuatiliaji wa hali ya vyoo na unawaji wa mikono, kwa kutumia vibuyu chirizi vyenye maji safi na sabuni, na kuhakikisha taasisi zote na kaya zote zinakuwa na vyoo vyenye vifaa hivyo. mikono.
"Simamieni taasisi zote na wananchi katika maeneo yenu, na kuhakikisha maeneo yote yana vyoo bora na si vyoo pekee bali vyoo vyenye vifaa vya maji yanayotiririka na sabuni ili kila mtu aweze kunawa mikono mara baada ya kutoka chooni" amesisitiza Ndelemo.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Afisa Afya halmashauri ya Arusha, Issa Msumari, amesema kuwa, licha ya kuwa, kwa sasa hali ya uwepo wa vyoo imeimarika kwa zaidi ya asilimia 90, lakini takwimu za hali ya unawaji mikono katika halmashauri hiyo, ni asilimia 35 tuu, jambo ambalo linatishia hali za afya na uwepo wa magonjwa ya kuhara, kuhara damu, magonjwa ya macho, magonjwa ya ngozi, maambukizi ya mfumo wa hewa yanayosababisha mafua pamoja na homa ya mapafu.
Awali maadhimisho hayo yaliambatana na burudani za vikundi mbalimbali zenye jumbe za uhamasishaji wa unawaji mikono, burudani zilizokwenda sambamba na masindano ya vikundi hivyo, ambayo kikundi cha maigizo, kutoka shule ya msingi Olchoki na Natema, waliibuka kidedea na kupata zawadi ya shilingi laki moja na elfu hamsini, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na shule ya kimnyaki na Selian, na nafasi ya tatu kuchukuliwa na shule ya msingi Loruvani na Moivo na washindi wa pili na watatu wote kupata fedha taslimu shilingi elfu hamsini.
Hata hivyo jumla ya shule za msingi 20 zimetunukiwa vyeti vya ushiriki katika maadhimisho hayo, kwa kuyapamba na kuwezesha wanafunzi na jamii iliyohudhuria, kufahamu umuhimu wa unawaji mikono unaozingatia hatua sahihi.
Uongozi wa Halmashauri ya Arusha, unawataka wadau mbalimbali kujitokeza kuhamasisha na kuwajengea wananchi uwezo wa umuhimu wa unawaji mikono na kuwashukuru wadau wa mashirika ya SNV, AceAfrica, WaterAid na Root&Shoots kwa kufanikisha maadhimisho hayo pamoja na kutoa elimu za afya ya jamii, katika halmashauri hiyo.
Maadhimisho ya siku ya unawaji mikono duniani, hufanyika Oktoba 15 kila mwaka, maadhimisho yaliasisiwa na shirika la Afya duniani (WHO) mwaka 2008, kwa mara ya kwanza Tanzania iliadhimisha mwaka 2011, kwa lengo la kuhamasisha, jamii kuongeza uelewa na ufahamu zaidi, umuhimu wa unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.