Na. Elinipa Lupembe.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa vitongoji vya Ngaramtoni na Emaoi kata ya Olmotony wameamua kutumia njia za kimila kuwatafuta wahalifu, walioiba vifaa kwenye miundombinu ya vituo vya kuchotea maji.
Kufuatia uharibifu na wizi wa vifaa hivyo, wananchi wamekubaliana kwa pamoja, kutafuta wezi hao kwa kutumia mila na desturi zao kimasai katika mkutano wa hadhara, uliojumuisha wananchi wa vitongoji hivyo, uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Ngaramtoni.
Wananchi hao baada ya majadiliano yaliyokuwa na hisia za kusikitishwa kutokea kwa vitendo hivyo vya kihalifu katika maeneo yao, wametoa kutoa siku saba kwa mtu au kikundi cha watu, waliohusika na wizi huo,kurudiasha vifaa hivyo na endapo havitarudishwa taratibu za kimili zitafuatwa.
Wananchi hao wamebainisha kuchoshwa na kusikitishwa na wizi mdogomdogo, unaoendelea katika jamii yao pamoja na tabia mbaya iliyojitokeza ya kuiba, hadi vifaa vilivyowekwa na wafadhili kwa ajili ya kuwaihudumia jamii yao.
Aidha wananchi hao wameonesha kuchukizwa na tukio hilo la wizi kwa kuwa mradi huo umegharamiwa na wafadhili kupitia serikali yao na kukiri kuwa mradi huo ni kwa faida yao, hivyo ni bora kuvunja chungu ili kukomesha tabia hiyo.
"Sisi wananchi wa Ngaramtoni tumechoshwa na adha ya maji, leo mfadhili kajitokeza ili tupate huduma ya maji, watu wanaharibu na kuiba vifaa, hatutakubaliana na tabia hiyo na ili kuikomesha tuvunje chungu" wamesema wananchi hao.
Akitangaza makubaluano hayo,Mwenyekiti wa kitongoji cha Emaoi Mh. Obed Kaipuk ametoa siku saba kwa wananchi kurudisha vifaa hivyo au kwa mtu yoyote aliyeona au kufahamu wahalifu hao na kuwataja kwa siri.
Ameongeza kuwa endapo siku saba zitapita bila wahalifu hao kujitokeza, siku ya tarehe 04.07. 2018, viongozi watakutana na wazee wa mila na kufanya taratibu za kuvunja chungu hicho.
Naye, Esuvati Meikara, mkazi wa kitongoji cha Ngaramtoni amethibitisha, kuwa kupitia imani ya kabila la kimasai ya kuvunja chungu, ni lazima wahalifu hao watajitokeza na kurudisha vifaa hivyo, na kila mmoja atakuwa mlinzi wa miundombinu hiyo ya maji.
Awali mratibu wa mradi wa shirika la WaterAid Arusha na Manyara, Upendo Muntambo, amesema kuwa licha ya kuharibu miundo mbinu hiyo lakini wezi hao wamefanikiwa kuiba betri na sola kwenye vituo sita, vifaa vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni sita.
Uongozi wa halmashauri ya Arusha, unawataka wananchi wote kuthamini na kuilinda miradi yote inayotekekezwa na serikali, kwenye maeneo yao pamoja na kutambua kuwa miradi hiyo ni mali ya umma na si mali ya mtu yoyote binafsi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.