Na. Elinipa Lupembe.
Wanafunzi wenye vipaji vya michezo, wametakiwa kushiriki michezo, inayoendeshwa kwenye shule zao, kwa kuwa ni sehemu ya taaluma itakayowawezesha kupata fursa ya kupata ajira hapo baadaye, pamoja na kukuza taaluma na kuimarisha afya zao.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, wakati akifungua mashindano ya michezo kwa shule za msingi - UMITASHUMTA, ngazi ya Halmashauri, ufunguzi uliofayika kwenye viwanja, vya shule ya Sekondari ya Ilboru, kwa lengo la kupata timu itakayoshiriki mashindano hayo ngazi ya mkoa.
Mkurugenzi huyo, amefafanua kuwa, licha ya kuwa michezo ni afya na inakuza taaluma, michezo pia ni fursa kubwa inayomuwezesha mchezaji, kupata ajira yenye maslahi mazuri ndani na nje ya nchi, na kuwasisitiza wanafunzi wenye vipaji kushiriki kwenye michezo inayoendeshwa shuleni kwa sasa.
Dkt. Mahera, ameongeza kuwa Serikali, imeona umuhimu wa michezo na kuamua, kurudisha michezo na mashindano kuanzia ngazi ya shule za msingi, ili kukuza vipaji vya wachezaji tangu wakiwa na umri mdogo, pamoja na kuwaanda wanafunzi wenye vipaji kupata ajira kwenye sekta ya michezo hapo baadaye.
"Michezo kwa sasa ni sehemu ya ajira tofauti na zamani, wapo wachezaji wanalipwa pesa nyingi, pengine kuliko wafanyakazi wengine, na imesaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa ajira kwa vijana katika taifa letu, hivyo Serikali ikaona ni vema michezo irudishwe shuleni" amesema Dkt Mahera
Aidha amewasihi wachezaji watakaochaguliwa, kufanya juhudi na kuwa na nidhamu wawapo kambini, ili kuiwakilisha halmashauri vizuri kwenye mashindano ngazi ya Mkoa na baadaye ngazi ya taifa.
Naye Afisa elimu Msingi, Mwalimu, Hossein Mghewa, amewataka wazazi, kuwapa watoto nafasi ya kuonyesha vipaji vyao, kwani michezo huburudisha, hujenga nidhamu, afya, umoja na hatimaye kuongeza kipato kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, mwanafunzi Zahara Khaleed wa shule ya Msingi Ngaramtoni, anayecheza mpira wa miguu, amethibitisha kuwa, michezo inawajengea uwezo wa kujiamini, nidhamu, huimarisha afya pamoja na kukuza mahusiano mazuri kati yao, na shule moja na nyingine, na kuwataka wazazi kuwaruhusu watoto wao, kushiriki michezo wawapo shuleni.
"Michezo inatusaidia kielimu, tunafundishwa nidhamu na kuimarisha Afya zetu, zaidi inatusaidia kutujengea mahusiano mazuri kati ya shule yetu na shule zingine na kutufanya tuishi kwa pamoja" amesema Mwanasoka huyo.
Awali, Mratibu wa Michezo ya UMITASHUMTA, Halmashauri ya Arusha, Mwalimu, Khalifa Kiyembe, amesema kuwa, mashindano ya UMITASHUMTA yalianzia ngazi ya kata kwa kushindanisha shule kwa shule na mpaka sasa jumla ya wachezaji 400 wamefanikiwa kufikia, ngazi ya halmashauri, kupitia wachezaji hao na timu zao, watachaguliwa wachezaji bora 100, kuiwakilisha halmashauri kwenye ngazi ya mkoa.
Mwalimu Kiyembe amebainisha kuwa, mashindano ya UMITASHUMTA mwaka 2019, yenye kauli mbiu ya 'Michezo na Sanaa kwa Elimu bora na Ajira', yanashirikisha mpira wa miguu kwa wavulana na wasichana, mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa mikono, riadha, mpira kwa wenye uono hafifu, pamoja na waimbaji.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.