Na. Elinipa Lupembe.
Wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka 2018, waishio kata ya Odonyowasi, Halmashauri ya Arusha, wameepukana na adha ya kutembea umbali mrefu, mara baada ya serikali, kuwapangia kujiungana elimu ya sekondari, katika Shule mpya ya Sekondari Oldonyowasi iliyopo ndani ya kata yao.
Awali wanafunzi wa kata hiyo, walilazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 16 kwenda na kurudi, katika shule ya Sekondari Oldonyosambu iliyopo kata jirani ya Odonyosambu, jambo ambalo wazazi wengi waliliona kusababisha wanafunzi wengi, kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao, huku wengine wakishindwa kuendelea na masomo na kuacha shule kabisa kutokana na kukatishwa tamaa na umbali.
Wanafunzi hao wamepata neema hiyo, baada ya wazazi na wakazi wa kata ya Oldonyowas, kuamua kuanza ujenzi wa shule ya sekondari na kuomba msaada kwa wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) pamoja na Serikali kupitia mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Akizungumza na mwandishi wetu shuleni hapo, Mwenyekiti wa kijiji cha Oldonyowas, mheshimiwa Geophray Ayo, amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo mpya ya Oldonyowas, ulianza mwaka 2018, mara baada ya wazazi kukerwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wao, hususani ya kutembea umbali mrefu kwenda kupata elimu ya sekondari.
Amesema kuwa, ujenzi ulianza kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na TANAPA kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na vyoo pamoja na samani za ofisi na za madarasa kwa gharama ya shilingi milioni 70 huku TANAPA wakitoa milioni 50 na wananchi milioni 15.
Ameongeza kuwa serikali kupitia miradi wa TASAF awamu ya III, haikusita kuunga mkono juhudi za wananchi wa Oldonyowas, kwa kuongezea nguvu na kufanikiwa kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi ndogo ya walimu, nyumba ya walimu yenye sehemu mbili (2 in 1), vyoo na jengo la utwala pamoja na kununua samani za ofisi na madarasa kwa, mradi uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 229.4, na kuwezesha shule hiyo kupata usajili milioni 229.4 na kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2019.
Hata hivyo mwenyekiti huyo ameendelea kueleza kuwa, wananchi wa oldonyowas wamekwenda mbali zaidi na kukusanya nguvu na kujenga jengo la maabara za masomo ya Sayansi, jengo lililogharimu shilingi milioni 45 kwa wananchi kuchangia shilingi laki moja kwa kila familia, jengo ambalo liko kwenye hatua za umaliziaji na kufanya shule hiyo kuwa na majengo saba yenye vyumba 6 vya madarasa, maabaara, vyoo, na nyumba ya walimu.
Licha ya kuishukuru serikali kupitia shirika lake la TANAPA na mradi wa TASAF kwa kusaidia ujenzi na usajili wa shule hiyo, amewashukuru pia wananchi wa Oldonyowas kwa kuchangia maendeleo ndani ya kata yao, pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya kutoa elimu bila malipo mpaka kidato cha nne, fursa inayowawezesha watoto wengi kuendelea na shule pindi wanapomaliza elimu ya msingi.
"Ninaishukuru serikali kwa niaba ya wananchi wa Oldonyowas kwa kuiwezesha shule yetu kusajiliwa na kupangiwa wanafunzi, na zaidi ninawashukuru wananchi wangu wa Oldonyowas, kwa kujitoa kwa hali na mali, kuhakikisha shule hii, inajengwa na kuanza kupokea wanafunzi kwa wakati kama tulivyopanga."ameshukuru Mwenyekiti huyo.
Naye Mkuu wa shule mpya ya sekondari ya Oldonyowas, mwalimu Richard Mugabuso, amesema kuwa shule hiyo imesajiliwa kwa namba *S.5111* mwaka 2018, na mwaka 2019 kupangiwa jumla ya wanafunzi 177, wanafunzi 166 walichukua fomu za kujiunga, mpaka sasa jumla ya wanafunzi 147 wameripoti na kuanza masomo, ikiwa ni wasichana 86 na wavula 61, huku zoezi la kupokea wanafunzi bado linaendelea.
Aidha mkuu huyo wa shule amezitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo mpya, ni pamoja na bado baadhi ya wanafunzi wanatoka mbali kwa kutembea takribani Kilomita kumi, uchache wa walimu, na nyumba za kuishi walimu na kuwataka wazazi kuanza kufikiria mikakati ya kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi hata kwa kuanza na watoto wa kike.
Halmashauri ya Arusha inawapongeza wananchi wa Oldonyowas kwa jitihada kubwa za kimaendeleo zinazofanyika kwa kujitoa kwa hali na mali kuibua na kushiriki kutekeleza miradi kwa ajili ya maendeleo yao na vizazi vyao, katika kata yao na kuwataka wananchi wa maeneo mengine kuiga mfano wa wananchi wa Oldonyowas, zaidi halmashauri, inawataka wadau wote wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono juhudi za serikali kwa kusaidia kuongeza miundombinu ya shule hiyo ikiwemo, mabweni, maktaba na vyumba vya madarasa.
Vyumba viwili vya ma, jengo linalojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF awamu ya III
Nyumba , walimu yenye sehemu ya kuishi familia mbili (2 in 1) jengo linalojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF awamu ya III.
Vyumba viwili vya madarasa na ofisi ndogo ya walimu, jengo linalojengwa na wananchi kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi ya Taifa - TANAPA.
Jengo la Maabara ya masomo ya Sayansi, linalojengwa kwa nguvu za wananchi wa Oldonyowas.
Jengo la choo walimu
Choo cha wanafunzi
Vyumba vya madarasa
Maeneo ya shule mpya ya sekondari Oldonyowas
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.