Na. Elinipa Lupembe.
Jumla ya shule nane za Msingi, halmashauri ya Arusha zimenufaika na mpango wa mafunzo kazini, unaotelewa na shirika la Inter- cooperation ( HELVETAS) la nchini Uswis kupitia Mradi wake wa Uboreshaji Elimu kwa mpango wa Mwalimu Mahiri (QUEETS), mradi unaotoa mafunzo kwa walimu waliopo kazini kwa masomo ya msingi, Hisabati, Kiingereza na Sayansi.
Walimu kutoka shule hizo nane, za Naurei, Sekei, Bangata, Laroi, Ng'ires, Nambere, Oldadai, na Olgilai, wameweza kupatiwa mafunzo ya mbinu mpya na rahisi za ufundishaji, pamoja na utengenezaji wa zana za kufundishia na kujifunzia, zinazotokana na mazingira wanayoishi.
Wakizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa elimu wa mradi huo, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, makao makuu ya CWT mkoa wa Arusha, walimu hao wamethibitisha kupata utalamu wa mbinu bora za kufundishia na kujifunzia, mbinu ambazo hazimchoshi mwalimu na mwanafunzi, huku zikiwajengea wanafunzi uwezo wa kuelewa na kumbukumbu ya muda mrefu wa kitu walichojifunza.
Katika kikao hicho, Mwalimu Athman Makale wa shule ya msingi Sekei kata ya Kiutu, amesema kuwa, mpango huo wa mafunzo umewafanya walimu kupenda kazi yao na kumudu kufundisha masomo hayo matatu kwa umahiri zaidi, jambo ambalo hapo awali walimu wengi walikwepa kujifundisha masomo hayo kwa kuyaona kuwa ni magumu.
Ameongeza kuwa licha ya mpango huo kuwawezesha kufanya kazi yao ya ufundishaji kwa umahiri mkubwa, mafunzo hayo yamewawezesha kujiamini na kuwa na uhusiano mzuri kati ya walimu na wanafunzi, kutokana na kutumia zaidi njia shirikishi inayowafanya wanafunzi kupenda masomo.
"Mpango huu wa mafunzo umetuwezesha walimu kufundisha kwa kushirikiana kama timu, umetufanya kujiamini kwa kile tunachofundisha, pamoja na kuwa na uhusiano wa karibu na wanafunzi, kwa kuwa muda mwingi tunawashirikisha wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi" amesema mwalimu Makale
Denis Elisha, mwanafunzi wa shule ya Msingi Naurei, amesema kuwa, kwa sasa walimu wao wanawafundisha kwa vitendo zaidi na kutumia zana za kufundishia, huku wakiwapa nafasi wanafunzi hao kufanya mazoezi ya jambo wanalojifunza wakati wa somo linapoendelea pamoja na kuwafundisha lugha ya kiingereza kwa kiingereza tofauti na hapo awali.
Ameongeza kuwa zamani walimu wao walikuwa wakiingia darasani na kuwafundisha kwa kuongea mwanzo mpaka mwisho na kuondoka bila kujali wameelewa au hawajaelewa, jambo ambalo lilikuwa linawapa wakati mgumu wanafunzi hao kuelewa walichojifunza, lakini sasa walimu hao huwashirikisha kuanzia utengenezaji wa zana za kujifunzia, wakati wa tendo zima la kujifunza wawapo darasani na kuhakikisha wameelewa.
"Walimu wetu zamani walikuwa hawako karibu na sisi, tulikuwa tunawaogopa, unakuta mwalimu anaingia darasani anafundisha kwa kuongea mwenyewe mwanzo mpaka mwisho wa kipindi, anamaliza na kuondoka bila kujali tumeelewa au la, lakini sasa tunawapenda walimu wetu, tunashirikiana hadi kutengeneza zana za kujifunzia, tuko huru na walimu" amesema Denis.
Afisa Elimu halmashauri ya Arusha, Mwalimu Hossein Mgewa amesema kuwa mradi wa QUEETS , umesaidia kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha kwa kutumia zana rahisi na njia shirikishi jambo ambalo limesaidia kupanda kwa taaluma kwa shule za msingi, na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hasa wale wanaofanya mitihani ya taifa ya darasa la nne na la saba.
Naye Meneja wa Mradi wa shirika la HELVETAS, Donathian Marusu, amesema kuwa mpango huu wa mafunzo kazini kwa walimu, umekuja baada ya tafiti kubaini kuendelea kushuka kwakiwango cha elimu ya msingikulikochangiwa na ukosefu wa mafunzo ya uhakika kwa walimj wawapo kazini, hivyo QUEETS, ikajipanga kutoa mafunzo kwa walimu ili wawe mahiri katika ufundishaji wenye lengo la kutoa matokeo bora.
Awali shirika la HELVETAS kwa kushirikiana na Chama cha Walimu Tanzania - CWT kupitia mradi wa Uboreshaji Elimu kwa Mpango wa Mwalimu Mahiri ( QUEETS), umeweza kutoa mafunzo kwa walimu 5514 kutoka shule za msingi 1,838, Maafisa Elimu wa kata 266 kwenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa kamati kuu ya Mradi wa kuwaendeleza walimu (QUEETS) ambaye ni mbunge wa Urambo, Mhe. Magreth Sita (kushoto) akizungumza na walimu walionufaika na mafunzo kazini wakati wa mkutano wa wadau wa elimu mkoani Arusha.
Walimu walionufaika na Mradi wa kuwaendeleza walimu kazini (QUEETS) wakitoa shuhuda namna mradi huo ulivyowasaidia katika kubiresha ufundishaji wao, wakati wa mkutano wa wadau wa elimu mkoani Arusha.
Mwanafunzi wa Denis Elisa wa shule ya msingi Naurei akito ushuhuda wa namna mpango QUEETS ulivyowawezesha kushirikishwa na walimu wao na kuwasaidia kuelewa kwa njia rahisi.
Afisa Elimu Msingi, halmashauri ya arusha, mwalimu Hossein Mghewa akizungumza na kutoa ushuhuda namna mradi wa kuwaendeleza walimu kazini (QUEETS) ulivyosaidia katika kuboresha ufundishaji ulioongeza ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba, wakati wa mkutano wa wadau wa elimu mkoani Arusha.
Wanafunzi wa shule ya msingi Naurei wakijifunza kwa makundi kwa kutumia zana rahisi zinazopatikana kwenye mzaingira yao.
Wanafunzi wa shule ya msingi Naurei wakijifunza kwa makundi kwa kutumia zana rahisi zinazopatikana kwenye mzaingira yao.
Wanafunzi wa shule ya msingi Naurei wakijifunza kwa makundi kwa kutumia zana rahisi zinazopatikana kwenye mzaingira yao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.