Waalimu wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Arusha, wametakiwa kuendelea kujituma na kujitolea katika kufundisha kwa bidii ili kufikia malengo ya serikali ya ufaulu wa zaidi ya asilimia 80% kwa kidato cha nne na asilimia 100% kwa kidato Cha pili.
Akizungumza na walimu wa sule ya sekondari Mlangari, alipotembelea shule hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, Afisa Elimu Sekondari, Halmashauri ya Arusha Mwl. Menard Lupenza, amewataka waalimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuweka mbele uzalendo zaidi, ili wanafunzi waweze kuelewa wanachofundishwa na kupandisha kiwango cha taaluma kinachokwenda sambamba na ongezeko la ufaulu.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto zinazokabili tendo la kufunisha na kujifunza, mwalimu anapaswa kutumia ujuzi na maarifa yake yote, vinavyoambatana na mbinu na zana halisi za kufundishia ili kumfanya mwanafunzi kuelewa na kuwa na kumbukumbu za kutosha kwa kitu alichofundishwa.
"Mwalimu unapokuwa darasani unatakiwa kuacha changamoto zote nje ya mlango wa darasa, na kutumia ujuzi, maarifa na mbinu shirikishi wakati wote, bila kusahau matumizi ya zana halisi za kufundishi, jambo litakalorahisisha uelewa kwa wanafunzi pamoja na kumbukumbu " amesema Afisa Elimu huyo.
Aidha Afisa Elimu huyo, amewataka waalimu hao kufanyakazi kwa kushirikiana pamoja na kuheshimu sheria na taratibu zote za kazi na kutambua wajibu na majukumu yao ni kifundisha, na kuifanya kazi hiyo kwa weledi kwa kutumia rasilimali zilizopo, ili shule hiyo iweze kushika nafasi za juu kwenye mitihani ya kitaifa.
Hata hivyo, Afisa Elimu Vifaa na Takwimu, Idara ya Sekondari, halmashauri ya Arusha, Mwalimu Charles John, amewasihi wanafunzi kuweka jitihada zaidi kwenye masomo yao, na kutambua kuwa serikali inatumia gharama kubwa kwa kuwapatia elimu bila malipo, hivyo ni vema kutumia vizuri fursa hiyo adhimu waliyoipata, kwa kuwa haitarudi tena, waweze kujikomboa kifkra na kimaisha hapo baadae.
Naye mwalimu Kajiru Malaji, amesema kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na walimu za kuwafundisha wanafunzi wao, changamoto kubwa ni upungufu wa mabweni na wazazi kushindwa kuchangia chakula cha mchana kwa ajili ya watoto wao wawapo shule, jambo linalofifisha matokeo mazuri kwa shule hiyo.
Amewataka wazazi kuona umuhimu wa kushirikiana na walimu kwa kuhakikisha kila mtoto anapata chakula cha mchana awapo shuleni, pamoja na ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi wanaotembea umbali mrefu, jambo litakalopandisha kiwango cha taaluma shuleni hapo.
"Wapo wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kuja na kurudi shule, wapo watoto ambao wazazi hawachangii chakula cha watoto wao na kuwafanya kushinda njaa, jamba ambalo huathiri tendo la lujifunza kwa wanafunzi hao" amesema mwalimu Malaji.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mlangarini, wameahidi kutumia fursa waliyonayo kusoma kwa bidii, na kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mitihani yao, kuanzia mitihani ndani, ya kiwilaya, mkoa mpaka Taifa.
Queen Benaford mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo licha ya kushukuru uongozi wa Halmashauri hiyo kuwatembelea, na kuwakumbusha wajibu wao kama wanafunzi na kuahidi kufanya jitihada kwenye masomo yao na kuhakikisha wanafaulu mitihani yao kuanzia mitihani ya ndani mpaka ile ya kitaifa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.