Na. Elinipa Lupembe.
Moja ya mikakati ya Serikali ya awamu ya tano, ni kuweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia pamoja na usimamizi imara wa kuthibiti ubora wa shule, lengo likiwa ni kupandisha kiwango cha taaluma kwa shule, kwa kuweka mazingira rafiki kwa walimu, wanafunzi na wasimamizi wa elimu.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi, Ufundi na Teknolojia, inaendelea kutetekeleza mikakati hiyo, kupitia miradi ya Lipa Kutokana na Matokeo (Education Payment for Result' ‘EP4R’), kwa kuanza kutekeleza miradi ya ujenzi wa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule kwenye Halmashauri zake.
Halmashauri ya Arusha ni miongoni mwa Halmashauri 100 Tanzania, zilizopata fedha kiasi cha shilingi milioni 152, fedha za Serikali kupitia miradi yake ya ‘EP4R’, ujenzi utakaogharimu kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Uthibiti Ubora wa Shule, Ofisi ambayo kwa kiasi kikubwa, itatatua changamoto ya msongamano wa wafanyakazi wa wa kitengoe hicho.
Mhandisi wa Ujenzi Halmashauri ya Arusha, Mhandisi Bibie Manzi, amesema kuwa, mradi wa ujenzi wa miundo mbinu ya Ofisi hiyo ya kisasa, uliozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, upo katika hatua za awali, mpaka kukamilika utagharimu kiasi cha shilingi milioni 152, na unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Augusti 2019, ukiwa umejumuisha vyumba vinne vya ofisi, ukumbi mdogo wa mikutano, jiko, vyoo pamoja na vyoo maalum kwa ajili ya watu wenye walemavu.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule, Halmashauri ya Arusha, Mwalimu Fatuma Lema, amesema kuwa, mradi huo wa ujenzi wa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule, katika halmashauri hiyo, umekuja wakati muafaka, kutokana na ufinyu wa ofisi iliyokuwa ikitumiwa na kitengo hicho kwa muda mrefu sasa, jambo ambalo lilisababisha kukwamisha ufanisi wa kazi.
“Kukamilika kwa mradi huo, kutaondoa changamoto nyingi zilizokuwa zinatokana na ufinyu wa ofisi tuliyokuwa inatumika, na zaidi kutaongeza ufanisi katika kazi za usimamizi wa utoaji elimu na kuthibiti ubora wa shuleni, pamoja na kuongeza ushirikiano baina ya wafanyakazi kwa kukaa kwa pamoja’amesema mwalimu Lema.
Akieleza shughuli zinazofanywa na kitengo cha Uthibiti Ubora ngazi ya halmashauri, mwalimu Lema, amefafanua kuwa, Kitengo cha Uthibiti Ubira wa Shule, ni dira ya elimu katika shule, kinachojishughulisha na kusimamia Sera ya Uthibiti Ubora wa Shule, kwa kusimamia ubora wa shughuli zote zinazofanywa shuleni, ikiwemo njia na mbinu sahihi za kufundishia, kufundisha kwa kufuata mitaala ya elimu, kuandaa masomo na nukuu za somo, pamoja na mazingira yote ya kujifunzia na kufanya tathmini ya ubora wa taaluma inayotolewa shuleni na kufanya tathmini ya kiwango na ubora wa elimu.
"Kitengo cha Uthibiti Ubora ni kitengo nyeti, kwani ndio Dira ya ubora wa shule, chenye jukumu la kusimamia utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi, matumizi ya mbinu sahihi za kufundisha na kujifunzia pamoja na kufanya tathmini ya ubora wa taaluma inayotolewa shuleni" amefafanua mama Lema.
Aidha mwalimu Lema, ameipongeza Serikali ya awamu ya tano, kwa kuona umuhimu wa kitengo cha Uthibiti Ubora wa Elimu, kwa kujenga ofisi, jambo ambalo halikuwahi kufanyika hapo awali, na kusababisha watumishi wa kitengo hicho, kujibanza kwenye ofisi za elimu.
Mwalimu Lema hakusita kumshukuru Murugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Arusha Dk. Wilson Mahera pamoja na ofisi ya Mkuu wilaya ya Aumeru kwa kukubali kutoa eneo la kujenga Ofisi hiyo, sharti ambalo lilitolewa na Serikali, pamoja na ushirikiano wa hali ya juu wakati wote wa mchakato wa utekelezaji wa mradi huo.
Serikali kupitia miradi ya EP4R inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia, imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.5, kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule, kwenye Halmashauri 100 za Tanzania.
Ujenzi wa Ofisi hizo ni utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Malipo, inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano, kwa kuboresha miundombinu ya elimu nchini, kwa lengo la kupandisha kiwango cha taaluma, na kurejesha hadhi ya shule za Serikali, iliyokuwa ikiendelea kupotea, kwa kuwezesha mazingira bora ya kujifunza na kufundishia na utoaji wa huduma ya elimu bora, mkakati ambao umeanza kuleta mafanikio chanya katika sekta ya elimu hususani uboreshaji wa miundombinu nchini.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.