Na. Elinipa Lupembe.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzani (TCRA), imeendelea kuimarisha miundombinu ya TEHAMA kwenye shule zinazoshika nafasi za juu kitaifa nchini, kwa kutoa motisha ya seti za Kompyuta kwenye shule hizo.
Shule ya sekondari Ilboro, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru ni miongoni mwa shule tano bora, zilizonufaika na mpango huo, kwa kupata seti komputa kumi na kutengenezewa tovuti ya shule, kwa kuweza kukidhi vigezo hivyo vilivyowekwa na TCRA, vifaa vitaksvyotumika kujifunzia somo la TEHAMA kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega licha ya kuishukuru TCRA kwa msaada huo wa Kompyuta, amewapongeza walimu na wanafunzi kwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa, na kuwataka walimu na wanafunzi kuvitunza vifaa hivyo, pamoja na kuvitumia kwa matumizi sahihi ya kujifunzia kama iliyokusudiwa na Serikali.
Ameeleza kuwa, kwa miaka minne mfululizo shule za mkoa wa Arusha zimekuwa zikifanya vizuri na kuufanya mkoa wa Arusha, kuingia kwenye kumi bora katika mitihani ya madarasa yote yanayofanya mitihani ya taifa, ikiwemo darasa la nne na la saba, kidato cha pili, cha nne na cha tano.
Ameongeza kuwa, anategemea sasa shule ya Ilboru, itafanya vizuri zaidi na kushika nafa si ya kwanza, kutokana na urahisi wa kujifunza kwa kutumia teknolojia ya kisasa kupitia Kompyuta hizo.
"Kama wakati wa analojia, Iboru ilikuwa kwenye shule tano bora, kupitia teknolojia ya dijitali, sasa Ilboru itakuwa Tanzania one" amesema Katibu Tawala huyo.
Naye Mkurugenzi wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Imelda Salum, amesema kuwa TCRA, imetoa vifaa hivyo vya kujifunzia kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia kompyuta kwenye masomo yao na kurahisisha tendo la kujifundisha na kujifunza.
Ameongeza kuwa, licha ya kuwa jukumu la TCRA ni kuhakikisha wananchi wote wanapata mawasiliano, lakini pia wana mkakati wa kutoa vifaa vya TEHAMA kwenye sekta ya elimu, ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kutumia teknolojia hiyo wangali shuleni.
Aidha, Mhandisi Imelda ametaja vifaa walivyokabidhi shuleni hapo ni pamoja na seti kumi za compyuta za mezani ikiwemo 'monitor, serve na printer'pamoja na kutengeneza tovuti ya shule hiyo, ambayo itawezesha kuweka taarifa zote muhimu za shule, ikiwemo matokeo ya wanafunzi.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Alvera Ndabagoye, ameahidi kusimamia matumizi sahihi ya Kompyuta hizo na kuwataka walimu kuhakikisha zinawewezesha wanafunzi kupata maarifa ya msomo yao na kujifunza mambo ya msingi kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla na si vinginevyo.
"Tunafahamu mitandao ina taarifa nyingi mnoo, ni jukumu letu walimu, kuwaongoza na kuwasimamia wanafunzi, kutumia kwa mambo ya msingi na ya muhimu katika maisha yao, wanafunzi wekezeni muda wenu kujifunza mambo ya muhimu na si vinginevyo" amesisitiza mkurugenzi huyo.
Hata hivyo wanafunzi wa sekondari Ilboru, licha ya kuishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, wamesema kuwa wanatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya sasa, za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kujifunzia kwenye shule za serikali na kuongeza kuwa, Komputa hizo, zitawarahisishia tendo la kujifunza, jambo ambalo litapandisha taaluma yao pamoja na kuongeza kasi ya ufaulu kwa shule yao.
Naye mkuu wa shule ya sekondari Ilboru, mwalimu Denis Otieno, ameishukuru Serikali, kupitia TCRA kwa msaada huo mkubwa, ambao utawezesha wazazi/walezi, wanafunzi na jamii, kupata taarifa za shule ya Ilboru popote walipo kupitia tovuti ya shule, iliyotengenezwa na mamlaka hiyo.
Mpaka sasa jumla ya shule za sekondari 20 za serikali, halmashauri ya Arusha, zina maabara za Kompyuta jambo ambalo linaendelea kupandisha kwa kasi taaluma na kupanda kwa kiwango cha ufaulu kwa shule za serikali tofauti na hapo awali.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.