Kufuatia mikakati ya Serikali ya awamu ya tano, ya kujikita zaidi katika kupambana na kutatua changamoto sugu zinazowakabili wananchi wake, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji, imetoa mtambo maalumu wa kuondoa kiwango cha madini ya Floraidi yaliyozidi kwenye maji ya kunywa yanayoyatumia na wananchi wa kijiji cha Lemanda kata ya Oldonyosambu, halmashauri ya Arusha.
Mtambo huo umewashwa rasmi kwa majaribio, mara baada ya watalamu wa kampuni ya O2andB kuusimika kwenye eneo la shule ya msingi Oldonyosambu, tayari kwa kuanza kuchuja maji ili kupunguza kiwango cha madini ya Floraidi yaliyozidi kwenye maji.
Akizungumza wakati wa kusimika mtambo huo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, amethibitisha kupokea mtambo huo kutoka serikali kuu, mtambo unaojulikana kwa jina la CDI 'Capacity of Dionization system, mtambo uliotengenezwa na Kampuni ya O2andB ya chini Korea.
Amefafanua kuwa mtambo huo una uwezo wa kupunguza kiwango cha madini ya Floraidi yaliyozidi pamoja na chumvi kwanye maji, kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuchuja maji bila kutumia kemikali.
Hata hivyo Dk. Mahera amekiri kuwa, mtambo huo una uwezo wa kuchuja maji na kupunguza kiwango cha Floraidi kutoka miligram 18.7 kwa lita moja hadi kufikia miligram 0.37 kwa lita moja, na kuongeza kuwa ni dhahiri kuwa tatizo hilo linakwenda kwisha na kuleta matumaini mapya kwa wananchi wa Lemanda, wananchi ambao wamepata athari kubwa za kimwili na kisaikolojia kufuatia madhara yatokanayo na kunywa maji yenye madini ya Floraidi iliyozidi kwa miaka mingi.
" Madhara yatokanayo na Floraidi sasa yamefikia mwisho kwa wakazi wa Lemanda, tunategemea sasa wananchi kutumia maji safi na salama yasiyo na Floraidi kama ilivyokua hapi awali" amesema Mkurugenzi Mahera
Naye Diwani wa kata ya Oldonyosambu Mheshimiwa Raymond Lairumbe, ameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Magufuli kwa kusikia kilio cha wananchi wa Lemanda, ambao kimsingi wengi wao wamepata madhara makubwa sana kutokana na kutumia maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya Floraidi huku watoto wakiathirika zaidi mifupa ya miili yao kwa kupinda miguu na kuwa na vichwa vikubwa.
" Nichukue fursa hii kumpongeza mheshimiwa Rais, Doctor John Pombe Magufuli, kwa kuwaonea huruma wananchi wa Lemanda, na serikali ya awamu ya tano kwa ujumla, serikali inayowajali wananchi bila kubagua itikadi zao, leo Lemanda tumepata mtambo mwarobaini wa kuondoa madini ya Floraidi kwenye maji ni kama ndoto kwa wananchi wangu " amesema Diwani huyo.
Aidha amewataka wananchi wote wa kijiji cha Lemanda, kuhakikisha wanafika shuleni hapo kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya kupikia na kunywa, kwa kuwa madhara ya Floraidi yanatokana na kula chakula kilichopikiwa maji yenye madini hayo pamoja na kunywa maji.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Lemanda, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Lemanda, Gaspa Mollel amesema kuwa, mtambo huo ni muhimu na neema kwa wananchi wa eneo hilo kutokana na ukweli kwamba, wananchi walikuwa wamekata tamaa ya kupata maji safi na salama, huku akiahidi kuongoza wananchi hao kuutunza mtambo huo, pamoja na kuendelea kuwahamasisha wananchi, juu ya umuhimu wa wananchi hao kutumia maji hayo safi na salama.
Naye Msimamizi Mkuu, Maabara ya Ubora wa maji mkoa wa Arusha, Jovitus Kichumu amesema kuwa, kiwango cha madini ya Floraidi kwenye maji yanayopatikana Lemanda ni miligramu 18.7 kwa lita moja, kiwango ambacho ni kikubwa sana na kisichofaa kwa matumizi ya binadamu na kufafanua kuwa mtambo huo unauwezo wa kuchuja na kupunguza mpaka kufikia kiasi cha miligram 0.37 kwa lita kiwango ambacho kinakubalika kimataifa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.