Na. Elinipa Lupembe.
Shirika lisilo la kiserikali la Kilimanjaro Technology, limekabidhi jengo la choo cha kisasa aina ya *SWASH* , chenye jumla ya matundu kumi, ujenzi uliogharimu jumla ya shilingi milioni 28, katika shule ya Msingi Seliani kata ya Kimnyaki, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru.
Shirika hilo linalofanya kazi zake Jijini Arusha na lenye makao yake makuu nchini Marekani, lilifikia uamuzi huo, mara baada ya choo cha shule hiyo kutitia mwezi Oktoba mwaka uliisha wa 2018 na kujeruhi mwanafunzi mmoja wa darasa la kwanza huku baadhi ya wanafunzi wakinusurika kuzama.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa jengo hilo la choo, mara baada ya kukamilika, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mheshimiwa Jerry Muro, amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa msada huo, msaada ambao umebeba thamani kubwa, kwa ustawi wa elimu ya watoto wa shule ya msingi Seliani na wilaya kwa ujumla.
Ameongeza kuwa choo ni muhimu sana kwa afya za wanafunzi wawapo shuleni, na zaidi ni sehemu inayochochea tendo la kujifunza na kupandisha taaluma kwa wanafunzi, na kuwataka walimu kusimamia wanafunzi wao, kukitunza choo hicho kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya choo hicho.
Licha ya kuwapongeza wadau wanaojitokeza kuunga mkono juhudu za serikali ya awamu ya tano, Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi wote kushiriki kuimarisha miundombinu ya shule zilizopo katika maeneo yao jambo ambalo litasaidia utoaji na upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa taifa la Tanzania.
"Kipekee niwashukuru sana shirika la Kilimanjaro Technology na wadau wote kwa kutuunga mkono kwani moja ya kipaumbele cha serikali katika sekta ya elimu ni uimarishaji wa ujenzi wa miundombinu kwa shule zetu zote, ili kuwezesha kuwa na mazingira bora ya kujifunza kwa wanafunzi" amesema mkuu huyo wa wilaya .
Akikabidhi msaada huo wa jengo la choo cha kisasa, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Rais wa shirika la Kilimanjaro Technology, kutoka nchini Marekani, Bi. Laurel Werner amesema kuwa, wameamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuunga mkono kwa vitendo jitihada za serikali ya Tanzania, kuboresha Sekta ya Elimu ambayo imeanza kuonyesha mafanikio kupitia Sera ya kutoa elimu bila malipo, kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari.
Bi. Laurel, amesema kuwa, serikali kutoa elimu bila malipo, inawapa nafasi na haki watoto wote kupata elimu hata wale wasio na uwezo, hatua ambayo imewavutia na kulazimika kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli.
Naye Lesasi Lukumai, mkazi wa Kimnyaki, wameushukuru uongozi wa shirika hilo na kuongeza kuwa ujenzi w choo hicho, umewapa wazazi amani na kuwa na uhakika wa usalama wa afya za watoto wao wawapo shuleni kwa kutumia choo imara, bora na cha kisasa.
Hata hivyo mara baada ya uzinduzi wa jengo hilo, mkuu wa wilaya, amewaahidi wakazi wa eneo hilo kuwa, siku chachezijazo, watazindua choo kingine cha kisasa chenye matundu 20, ambacho kimejengwa Kwa ushirikiano wa wananchi, serikali pamoja na wadau wengine wa Maendeleo, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na changamoto ya kutitia Kwa choo cha shule ya msingi Seliani na kujeruhi mwanafunzi mmoja wa darasa la kwanza.
Naye Afisa Elimu ufundi,halmashauri ya Arusha, Mwalimu Sokoine Mollel amesema kuwa, uwepo wa vyoo vya kisasa shuleni licha ya kuwa na faida kubwa kiafya lakini pia huwezesha wanafunzi kurahisisha tendo la kujifunza na kufundisha na kufafanua kuwa jengo hilo la choo litatumiwa na watoto wa kike wa shule hiyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.