Na. Elinipa Lupembe.
Shirika lisilo la kiserikali la Aspiration for Vulnerable Rehabiltated Families (AVUREFA), litaanza rasmi kutoa huduma za afya za mkoba 'mobile clinic', kwenye maeneo ya pembezoni, katika halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, lengo likiwa ni kupambana na magonjwa sugu na kuwa na taifa lenye afya bora.
Akizungumza wakati wa kulitambulisha shirika hilo, kwenye kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa SOS, Mkurugenzi wa Shirika la AVUREFA, Dkt. Furaha Kitiwe, amethibitisha kuwa, shirika hilo litaanza kutoa huduma za afya za majumbani, kwa maeneo ya pembezoni kwa kuwahudumia wagonjwa walioathirika na ugonjwa wa UKIMWI na Kifua Kikuu, Utapiamlo, huduma za Afya ya Uzazi na uzazi wa mpango.
"Tutashirikiana na halmashauri kutoa huduma hizo, kupitia 'mobile clinic' kwa kuwafikia watu katika maeneo yao, lengo likiwa ni kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa sugu ya UKIMWI na TB, Kansa ya Mlango wa kizazi na kutambua dalili za awali, kuwapima, kutibu na zaidi kuzuia maambukizi kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu mwingine" amesema Mkurugenzi wa AVUREFA.
Aidha, Dkt. Kitili amefafanua kuwa, shirika litashirikiana na watalamu wa afya wa halmashauri hiyo, kuwafikia wagonjwa hao majumbani, na kutoa elimu ya maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, dalili zake, namna ya kujinga pamoja kuwafanyia vipimo, kutoa dawa, na namna ya kuwatunza wagonjwa hao na kuepuka unyanyapaa na maambukizi mapya pamoja na elimu ya lishe bora kwa wagonjwa hao.
Hata hivyo Dkt. Kitiwe amefafanua kuwa, shirika hilo limeamua kutoa huduma hizo za afya, kwa lengo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika sekta ya afya, hasa katika kuweka mazingira rafiki ya kuwahudumia wananchi na kuwafikia hasa wa maeneo ya vijijini.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa wilaya, Afisa Afya, halmashauri ya Arusha, Issa Msumari, amesema kuwa, halmashauri itashirikiana na shirika hilo, kuwahudumia wagonjwa hao, majumbani ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuwafikia wagonjwa hasa waishio maeneo ya pembezoni.
Ameongeza kuwa lengo la serikali ni, kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ili kuweza kufanyakazi na kujenga taifa, kwa kuwapatia elimu ya afya na magonjwa, sambamba na kuwapatia huduma bora za afya, pale wanaposhambuliwa na magonjwa, hivyo shirika hilo linatekeleza malengo halisi ya serikali.
Naye, Afisa Mtendaji wa kata ya Sambasha, Nkini amekiri, uhitaji wa huduma hizo za afya majumbani, kutokana na uelewa mdogo wa jamii, juu ya ugonjwa Kifua Kikuu na maambukizi, namna ya kujikinga na namna ya kuwahudumia wagonjwa hao pamoja na lishe bora kwa wagonjwa, jambo ambalo linasababisha ongezeko la wagonjwa na pengine vifo.
"Bado jamii haina uelewa wa kutosha juu ya ugonjwa wa TB, dalili za ugonjwa huo, kuchelewa kwenda hospitali kupata vipimo, jambo linalosababisha maambukizi kutokea, kupitia huduma hizo, tutaweza kuokoa maisha ya watu wengi zaidi" amesema Afisa Mtendaji huyo.
Awali, shirika la AVUREFA linaanza kutekeleza mradi huo wa awali kwa kipindi cha miezi sita kuanzia sasa, kwa kuanza na kata ya Sambasha na baadaye kuendelea maeneo mengine ya pembezoni ya halmashauri hiyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.