Na. Elinipa Lupembe.
Wajumbe wa Baraza la madiwani, halmashauri ya wilaya ya Arusha, wilayani Arumeru wamepitisha rasimu ya makadirio ya mpango wa bajeti wa mapato na matumizi kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020, huku asilimia 15 ya bajeti hiyo ikijikita kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha rasimu hiyo ya mpango wa bajeti, katika mkutano maalumu wa baraza la madiwani, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, ameeleza kuwa, katika mwaka wa fedha ujao wa 2019/2020, halmashauri ya Arusha imekadiria kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 50.8, huku bajeti hiyo ikijikita kwenye ukomo ule ule wa makisio ya mwaka wa fedha 2018/19, kukiwa hakuna ongezeko lolote la fedha.
Mkurugenzi huyo, ameainisha mchanganuo wa makadirio hayo ya mapato na matumizi wa bajeti hiyo, kwa kuwaelezea wajumbe kuwa, kiwango hicho cha fedha kitatokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo, mapato ya ndani, mishahara pamoja na miradi ya maendeleo na kuweka bayana kuwa, kiasi cha shilingi bilioni 1.3 sawa na asilimia 2.92 kitatokana na mapato ya ndani, Ruzuku fidia ya mapato imekadiriwa jumla ya shilingi milioni 58 sawa na asilimia 0.16, Ruzuku ya matumizi mengine shilingi bilioni 1.5 sawa na asilimia 2.92.
Ameendelea kufafanua kuwa, kiasi cha shilingi milioni 39.9 sawa na asilimia 78.38 ikiwa ni Ruzuku ya mishahara na kiasi cha shilingi milioni 38.3 sawa na asilimia 0.08 ikiwa ni mishahara itakayotokana na mapato ya ndani, huku kiasi cha shilingi bilioni 8.07 sawa na asilimia 15 kikielekezwa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, halmashauri inategemea kutumia kiasi cha shilingi bilioni 8.07, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.6 ikiwa ni mchango wa halmashauri kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ya ndani na kiasi cha shilingi bilioni 4.3 ikiwa ni Ruzuku ya miradi ya maendeleo kutoka Serikali Kuu.
Dkt. Mahera ametaja mchanganua wa makadirio ya fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 8, kuwa ni pamoja na kiasi cha shilingi milioni 56.3 ikiwa ni fedha za Mfuko wa Jimbo sawa na asilimia 0.70, shilingi milioni 605.2 Mfuko wa afya wa pamoja - HSBF sawa na asilimia 7.50, shilingi bilioni 1.4 fedha za Ruzuku ya kuendeleza maji vijijini-NWSSP sawa na aslimia 17.66, Ruzuku ya elimu bila malipo kwa shule za Msingi shilingi milioni 831 sawa na asilimia 10.30, ruzuku ya elimu bila malipo sekondari shilingi bilioni 1.4 sawa na asilimia 17.72, shilingi milioni 45 fedha za kampeni ya Usafi wa Mazingira sawa na asilimia 0.56 huku shilingi bilioni 3.6 sawa na asilimia 45.67 ikiwa ni fedha za Mapato ya ndani.
Aidha Mkurugenzi Mahera amesisitiza kuwa, katika rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, halmashauri imepanga kutekeleza majukumu yake ya msingi yenye lengo la kutoa huduma bora na kuondoa umasikini kwa wananchi wake kupitia vipaumbele vyake kwa kushirikiana na wananchi, Serikali kuu na wadau wa maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo na ushitika, mifugo na uvuvi, ardhi, maliasili na mazingira, rasilimali watu na TEHAMA.
Licha ya halmashauri kukabiliwa na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa mapato,halmashauri imejipanga kubuni vyanzo vipya vya mapato huku ikiendelea kushirikisha jamii katika ulioaji wa kodi na ushuru mbalimbali.
Hata hivyo, baada ya mjadala mrefu na wa kina, wajumbe wa baraza la madiwani, wameridhia mapendekezo ya rasimu hiyo ya mpango wa makadirio ya mapato na matumizi yaliyowasilishwa, kutokana na uhalisia wa bajeti hiyo kujikita kwenye sekta zote,zaidi ikielekeza kujikita katika kutoa huduma bora kwa jamii na kuondoa umasikini na kuahidi kutoa ushirikia kwa watalamu katika kutekeleza bajeti hiyo.
Diwani wa kata ya Musa, mheshimiwa Flora Zelote amesema kuwa, mapendekezo ya rasimu ya bajeti yanaridhisha kwa kuwa umbile la bajeti limegusa maslahi mapana ya jamii hususani afya, elimu, usalama wa raia na miundombinu na haki za binadamu.
Mara baada ya rasimu hiyo kupitishwa, halmashauri imeahidi kutekekeleza bajeti hiyo kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi na kwa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kutumia mashine za kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.