Somo la teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA limezidi kuimarika katika shule za sekondari 14 za halmashauri ya Arusha baada ya wafadhili kusimamia na kutoa kompyuta kwa shule hizo.
Uimara huo umetokana na ufadhili thabiti wa shirika lisilo la kiserikali la Reneal Intanatinal Education Outreach la nchini Marekani kufadhili ufundishwaji na uendeshwaji wa somo la TEHAMA katika shule hizo.
Kwa kipindi cha takribani miaka mitano sasa kuanzia mwaka 2013, Shirika hilo limewezesha uwepo wa Maabara za Kompyuta kwenye shule 14 na kutoa kompyuta 300 na viambata vyake kwa awamu tofauti huku idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hizo wakifaidika.
Akizungumza wakati wa kufungua maabara mpya ya komputa kwenye shule ya sekondari Sokon II na kukabidhi komputa 17 za maabara ya shule hiyo, mkurugenzi na mwanzilishi wa shirika hilo, Bibi Rene Bierbaum amesema kuwa, wanafarijika sana kuendelea kutoa vifaa hivyo kwenye shule za sekondari katika halmashauri ya Arusha, kutokana na ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa uongozi wa halmashauri hiyo, usimamizi imara wa komputa hizo shuleni pamoja na mwamko wa wanafunzi kutumia komputa hizo kama zana za kujifunzia.
Bibi Rene ameongeza kuwa, katika awamu hii ya mwisho, Reneal imetoa jumla ya Komputa mpakato 68, Kwa mgao wa kompyuta 17 kwa kila shule kwa shule nne za sekondari za Skon II, Kiranyi, Kimnyaki na Oldonyosambu, na kuongeza kuwa komputa 47, zimeongezwa kwenye shule ambazo zilipata mwanzo na baadhi kubadilishwa zile ziliokaa kwa muda mrefu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dk. Wilson Mahera, licha ya kulishukuru na kulipongeza shirika la RENEAL kwa msaada huo, amewataka walimu na wanafunzi kuzitunza kompyuta hizo na kusisitiza kutumika hasa kwa ajili ya kujifunzia mambo muhimu ya kimasomo pamoja na kuhakikisha zana hizo zinaleta matokeo mazuri kwenye mitihani yao ya ndani na ile ya taifa.
Hata hivyo amefafanya kuwa mkakati wa halmashauri ni kuhakikisha shule zote za sekondari zinakuwa na maabara za Kompyuta ili kuwezesha wanafunzi wote kufanya mitihani ya Taifa ya somo la TEHAMA kuwa na ufaulu wa juu wa somo hilo na kuwa wabobezi katika matumizi ya kompyuta.
"Ingawa tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule zetu, mkakati wetu ni kushirikiana na wadau Reneal na wadau wengine kuhakikisha ifikapo mwa 2020 shule zote 27 za sekondari kuwa na maabara za kompyuta na wanafunzi wote kuweza kufanya mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na cha nne kwa somo la TEHAMA huku wakiwa na uwezo mkubwa wa kutumia kompyuta" amesema Mkurugenzi Mahera.
Mkuu wa shule ya Sekondari Sokon II,mwalimu Mwamvita Kilonzo, amethibitisha kuhakikisha kompyuta hizo, zinatumika katika matumizi sahihi kwa wanafunzi kwa kujikita zaidi katika kujifunza kutumia kompyuta, kujifunza somo la TEHAMA na kutumia kama zana ya kujinzia kwa kupata Nukuu za mosomo mengine kupitia mtandao wa intaneti huku akisisitiza kuzuia matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wanaunzi watakaotumia kompyuta hizo.
Naye Mratibu wa mradi huo wa maabara za Kompyuta shule za sekondari na Afisa TEHAMA, halmashauri ya Arusha David Nyangaka, amesema kuwa Kompyuta hizo, hazitakuwa na mfumo wa mitandao ya kijamii bali zimejazwa mambo ya muhimu yanayohusiana na masomo ya sekondari hivyo kuwafanya wanafunzi kutumia kwa ajili ya masomo zaidi na maarifa mengine ya ziada yanayoendana na maadili ya kitanzania na si vinginevyo.
Mkurugenzi Mtendaji Dk. Wilson Mahera kushoto, mkuu wa shule sekondari Sokon II mwalimu Mwamvita Kilonzo pamoja na mwenyekiti wa kijiji cha Sokon II mheshimiwa Melau Mollel wakizitazama baadhi ya kompyuta mpakato mara baada ya kukabidiwa na wadau wa shirika la Reneal.
Mkurugenzi na mwanzilishi wa shirika la RENEAL INTERNATIONAL EDUCATION OUTRICH BibiRene Bierbaum akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Sokon II.
Wakurugenzi na waanzilishi wa shirika la RENEAL INTERNATIONAL EDUCATION OUTRICH Bwana Neal Bierbaum na Bibi Rene Bierbaum wakimkabidhi kompyuta mpakato Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Sokon II wakicheza ngoma ya kabila la Kimaasai, wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa maabara mpya ya kompyuta pamoja a kukabidhiwa kompyuta na shirika la Reneal.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Sokon II wakiwa kwenye maabara yao mpya ya kompyuta mara baada ya kufunguliwa na kukabidhiwa kompyuta 17 na shirika la Reneal International Education Outrich.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.