Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, mheshimiwa Mrisho Gambo, amewataka Maafisa Watendaji wa Kata na vijiji, wilayani Arumeru kulipa umuhimu zoezi la ugawaji vitambulisho vya wajasiriamali, alipokutana nao kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri ya Arusha.
Mkuu huyo wa mkoa, ametoa wito huo alipokutana na watendaji hao wa halmashauri za Arusha na Meru zinazounda wilaya ya Arumeru na kuwakabidhi jumla ya vitambulisho elfu 24 kupitia Mkuu wa wilaya ya Arumeru, na kutoa muda wa mwezi mmoja, kuhakikisha wajasiriamali wote katika maeneo yao wamepata vitambulisho hivyo.
Mheshimiwa Gambo ametoa ufafanuzi, juu ya umuhimi wa zoezi hilo na kusema kuwa, lengo la serikali ni kutambua idadi ya wajasiriamali walio katika sekta isiyo rasm, kutokana na ukweli kuwa, wafanya biashara wengi wanakwepa kulipa kodi huku wafanya biashara wachache wakibeba mzigo wa kulipa kodi kila mwaka.
Kupitia vitambulisho hivyo, kutawezesha kutambulika kwa wajasiriamali walio katika sekta isiyo rasmi, kuweza kuwasimamia wajasiriamali hao kukua kwa kukuza mitaji ili na kuwawezesha kufikia ngazi ya wafanyabiashara.
"Wapo wafanyabiashara wasiojulikana popote, lipo kundi la wafanyabiashara limejificha, wao hawalipi kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania - TRA wala kulipa halmashauri, kupitia zoezi hili la utambuzi, serikali itawapata hao wanaojificha" amesema mheshimiwa Gambo.
Licha ya kuwa serikali imeweka mkakati wa kulitambua kundi hilo la wajasiriamali kwa kuwapa vitambulisho, lakini kumekuwa na upotoshaji juu ya vitambulisho hivyo, unaosababisha jamii kutokuelewa lengo la serikali la kugawa vutambulisho hivyo, na kushindwa kupima ni yupi mfanyabiashara na yupi ni mjasiriamali.
Hata hivyo Gambo amewata watendaji hao, kuhakikisha wajasiriamali wote katika maeneo yao, wanapatiwa vitambulisho ili kila mjasiriamali aweze kutambulika na kuweza kufanyabiashara yake kihalali bila kubughudhiwa.
"Niwatake watendaji msikae ofisini kusubiri wajasiriamali kuwafuata bali wafuateni kwenye maeneo yao na kuwasajili ili kufikia lengo la serikali la kupata data base ya wafanyabiashara wote" amesisitiza mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha amewataka Maafisa watendaji hao, kukusanya kodi ya majengo 'propert tax' ambayo serikali imeelekeza kila nyumba ya kawaida shilingi elfu 10 na ghorofa shilingi elfu 50, na kuagiza kila Afisa mtendaji wa kijiji kuorodhesha idadi ya nyumba katika kijiji chake ili kodi hizo zikusanywe na kupeleka TRA.
Naye Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mhe. Jerry Muro, ameeleza kuwa kwa awamu ya kwanza wilaya ya Arumeru imeshagawa vitambulisho 4500 kati ya 6000 kupitia maafisa biashara wa halmashauri ya Arusha na Meru, na kuonekana bado juhudi zinahitajika ili kuwafikia wajasriamali katika maeneo yao.
Hata Maafisa Watendaji hao wa kata na vijiji wamegawana vitambulisho hivyo, kulingana na idadi ya watu katika makazi, huku wale wa maeneo ya miji yakipatiwa idadi kubwa ya vitambulisho hivyo na kuahidi kwenda kuchapa kazi kwa kuwazungukia wajasiriamali katika maeneo yao.
Afisa Mtendaji kata ya Ngarenanyuki, Victor Kaijage amesema wakotayari kuanza rasmi zoezi hilo na kuahidi kufanya jitihada ili kuwafikia wajasiriamali wote katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kuwatembelea katika biashara zao ili kufikia lengo la serekali.
Wilaya ya Arumeru ina halmashauri mbili za Arusha na Meru ikiwa na kata 53 na vijiji, yenye jumla ya wakazi 591,342 kulingana na Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na ongezeko la asilimia 2.5, huku ikiwa pia na Mamlaka mbili za miji midogo USa na Ngaramtoni, miji inayokua kwa kasi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.