Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, mheshimiwa Mrisho Gambo, ameitaka Idara ya Maendeleo ya nchini Uingereza ' Department For International Development' (DFID) kujipa muda wa kufanya tafiti zaidi ya namna ya kuendesha mradi wa maji wa Vijiji vitano, mara baada ya mradi huo kukamilika na kukabidhiwa kwa serikali, kutokana na gharama kubwa za uendeshaji mitambo ya kuchuja maji, ili mradi huo uwe endelevu kama ulivyokusudiwa.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa rai hiyo ofisini kwake, alipokutana na ujumbe kutoka DFID - Tanzanzia, ujumbe uliolenga kutoa taswira halisi ya utekelezaji wa mradi huo wa maji, unaotekelezwa kwenye vijiji vitano ndani ya halmashauri ya Arusha na shirika la WaterAid Tanzani, kwa gharama ya shilingi bilioni 8.4.
Mheshimiwa Gambo ameweka wazi kuwa, mradi huo wa maji umesanifiwa kwa kutumia mitambo ya kisasa, yenye kuchuja maji na imetumia gharama kubwa, huku uendeshaji wa mitambo hiyo, ukitegemea kutumia gharama kubwa za uendeshaji na kuitaka DFID, kujipa muda zaidi wa kusimamia mradi huo mpaka kufikia hatua ambayo mradi huo utaweza kujiendesha.
"Mradi huu wa maji, umegharimu fedha nyingi na unatumia mitambo ya kisasa ya kuchuja maji, mitambo inayohitaji gharama kubwa za uendeshaji, niombe DFID hata baada ya mradi kukamili, kujipa muda wa kuendelea kushirikiana na serikali kusimamia uendeshaji wa mradi huo ili uweze kuwa endelevu" amesema mhe. Gambo
Ameongeza kuwa, wananchi wana maratajio makubwa kwenye mradi huo, kutokana na ukweli kwamba, wananchi hao wameteseka kwa adha ya maji kwa muda mrefu, kutokana na shida ya maji yenye madini ya floraidi, inayowakabili wananchi hao, na kusisitiza kuwa DFID wanapaswa kuangalia umuhimu wa mradi huo kwa wananchi pamoja na gharama kubwa walizotumia kutekeleza mradi huo.
Hata hivyo mwakilishi wa DIFID, Getrude Mapunda, licha ya kuishukuru na kuipongeza serikali kupitia uongozi wa mkoa wa Arusha, ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, halmashauuri ya Arusha na wadau wote wanaotekeleza mradi huo wa maji, amesema kuwa, wataendelea kushirikiana na serikali, wadau na wananchi kuhakikisha mradi huo mkubwa unakuwa endelevu kama ilivyo katika lengo na usanifu wa mradi.
Getrude amefafanua kuwa DFID, inafadhili miradi ya maji kwa lengo la kuhakikisha wananchi wapata maji safi na salama na kuongeza kuwa mradi huo wa vijiji vitano, umesanifiwa kutumia mitambo ya kuchuja maji na kuondoa madini ya floraidi na madini ya chumvi, mitambo ambayo imetumia gharama kubwa, lengo likiwa ni kuwapatia wananchi maji safi na salama na mradi kuwa endelevu.
Naye Mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania Dkt. Ibrahim Kabole, amemueleza mkuu wa mkoa kuwa, mradi huo ulianza mwaka 2017, kwa sasa uko katikz hatua za mwisho kukamilika, na wanategemea kukabidhi mradi huo ifikapo mwezi Machi, 2020.
Dkt. Kabole amefafanua kuwa mradi huo utakuwa na vituo 92 vya kuchotea maji na tayari vituo 46 vya kuchota maji vimeanza kutoa huduma, huku vituo vingine 41 vikiendelea na ukamilishaji, wakati huo huo, marekebisho madogo madogo yakiendelea kufanyika kabla ya wakandarasi kukabidhi mradi.
Mradi wa maji wa Vijiji vitano, umefadhiliwa na DFID na kutekelezwa na Shirika la WaterAidTanzania, unategemea kukamilka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wa 2020, na utahudumia takribani wananchi 50,000 wa vitongoji vya Ngaramtoni, Ekenywa, Seuri na vijiji vya Olkokola na Lengijave, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.