Na. Elinipa Lupembe.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Elimu Mheshimiwa, Mwita Waitara, ameahidi kushughulika changamoto ya maji na miundombinu ya barabara, zinazoikabili shule ya sekondari Mwandet, halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru.
Naibu Waziri, Waitara ametoa hadi hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea shule za sekondari Mwandeti na Mlangarini katika halmashauri hiyo, kwa lengo la kukagua miradi inayotekelezwa na Serikali, kupitia fedha za miradi ya Lipa kutokana na Matokeo 'EP4R', na kupata wasaa wa kuzungumza na wanafunzi, viongozi wa kata na bodi za shule hizo.
Ahadi hiyo imekuja, mara baada ya wanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Mwandet, kutoa kilio chao, cha uhaba wa maji shuleni hapo, ubovu wa barabara ya kuingia shuleni pamoja na upungufu wa nyumba za walimu, changamoto wanazodai wakati mwingine, zinawapotezea muda wa kujikita kwenye masomo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Dada Mkuu wa shule hiyo, Riziki Joseph, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa, katika eneo la shule yao hakuna maji, jambo linalowalazimu wanafunzi, kutumia muda mwingi kutafuta maji nje ya shule, jambo ambalo licha ya kuwapotezea muda wa kujifunza, pia ni hatari kwa usalama wa wanafunzi hasa wanafunzi wa kike.
Ameongeza kuwa, barabara ya kuingia shuleni hapo ni mbovu, wakati mwingine walimu kushindwa kufika shuleni hasa kipindi cha mvua, kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa nyumba za walimu na kukosekana nyumba za kupangisha kijijini hapo, jambo linalowalazimu baadhi ya walimu kuishi mjini zaidi ya Kilomita 30 kutoka shuleni hapo.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo, ameahidi kushughulika suala hilo, ili maji yaweze kupatikana shuleni hapo na kuhakikisha barabara hiyo inatengenezwa, ili kutimiza lengo la serikali la wanafunzi kupata elimu katika mazingira rafiki.
" Ninaahidi kwenda kuhughulikia suala la upatikanaji wa maji shuleni hapa, pamoja na matengenezo ya barabara ambayo hata mimi nimeiona sehemu ambayo daraja linakaribia kukatika muda wowote na kupoteza mawasiliano na kuzuia kuingia wala kutoka" ametibitisha Naibu Waziri Waitara
Aidha mheshimiwa Waitara, amewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa kujitoa, kuchangia miradi ya maendeleo katika shule zao, na kuwataka kuongeza kasi na kuendeleza mabweni mawili yaliyoanzwa kujengwa na serikali ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule hizo.
Naibu Waziri huyo pia ameushauri uongozi wa halmashauri ya Arusha, kufanya mawasiliano endapo wanakutana na changamito za kifedha na kimazingira, zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi, mara baada ya serikali kutoa fedha za miradi, badala ya kufanya maamuzi ya matumizi ya fedha hizo, ili kuepuka hoja za ukaguzi.
Katika shule hizo mbili, zaidi ya shilingi milioni 600 zimetumika kuendeleza miundombinu ya vyumba 12 vya madarasa na mabweni ya kidato cha tano na sita, ukamilishaji wa maabara za masomo ya Sayansi, ujenzi wa Maktaba, umaliziaji na ukarabati wa mabwalo ya kulia chakula pamoja na ujenzi wa vyoo.
Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI mheshimiwa Mwita Waitara akikagua jengo la Bwalo la kulia chakula wanafunzi wa shule ya sekondari Mwandet, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na fedha za miradi ya P4R.
Bwalo la chakula shule ya Sekondari Mwandet liko hatua za mwisho kukamilika baada ya Serikali kutoa shilingi milioni 60 fedha za P4R kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa bwalo hilo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.