Msamaria mwema na mwanzilishi wa shirika la kulelea watoto yatima la Neema Village, bwana Michael Fortson ametoa msaada wa vifaa maalum kwa ajilili ya walemavu wa ngozi, katika halmashauri ya Arusha.
Bwana Fortson ametoa msaada kwa walemavu hao wa ngozi baada ya kuona jinsi walemavu hao wanavyopata shida ya ngozi kwa kukosa mafuta hayo maalumu kwa ngozi zao.
Fortson amemkabidhi jumla ya chupa 71 za mafuta ya kujipaka, miwani 48 na kofia 48 kwa uongozi wa halmashauri huyo ili waweze kugawa vifaa hivyo,kwa walemavu hao ndani ya halmashauri.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Fortson amesema kuwa, anatambua madhara wanayoyapata walemavu wa ngozi endapo watakosa vifaa maalumu vya kujikinga na jua kama miwani, kofia na mafuta.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo, Afisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya Arusha, Beatrice Tengi amemshukuru bwana Fortson kwa kuunga mkono serikali ambayo kimsingi ndio imebeba jukumu hilo kubwa la kugharami vifaa vya walemavu wa ngozi, hasa wale wasio na uwezo.
Tengi amefafanua kuwa, walemavu wengi wa ngozi hushindwa kumudu gharama za kununua vifaa hivyo, kwa kuwa huuzwa kwa bei ghali kiasi cha mtu wa kawaida kushindwa kununua.
Ameongeza kuwa, kutokana na ufinyu wa bajeti halmashauri hutoa mafuta mara moja kwa mwaka , jambo ambalo husababisha wakati mwingine baadhi ya walema kuishi bila kupaka mafuta hayo maalumu, jambo ambalo linaweza kuwasababishia madhara.
" Baadhi ya walemavu wa ngozi hutegemea mafuta tunayowagawia kama halmashauri, ambayo tunayatoa mara moja kwa mwaka huku walemavu hao hutakiwa kutumia mafuta hayo siku zote za maisha yao" amesema Tengi.
Aidha Afisa Ustawi huyo, amewaomba wadau mbalimbali, kujitokeza kuwasaidia walemavu hao wa ngozi, kutokana na ukweli kwamba, wanahitaji misaada ya vifaa kwa kuzingatia hasa wengi wao wana hali duni za kimaisha.
Hata hivyo Tengi amethibitisha kuwa, tayari wameshaanza kuvigawa vifaa hivyo kwa wahusika, kila wanapokwenda kwenye kata na vijiji kikazi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.