Madaktari wa mifugo halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, wameanza mkakati wa kuthibiti mbwa kuzaliana kwa kuwafaniyi upasuaji wa kuhasi mbwa dume na kuwatoa vizazi mbwa jike kwa lengo la kupunguza mbwa wanaozurura mitaani na kuwa kero kwa wakazi..
Akizungumza na mwandishi wetu, daktari wa mifugo halmashauri ya Arusha, Dkt. Yohana Kiwone, amesema kuwa zoezi hilo ni la kawaida kufanyika kwa mifugo aina ya mbwa ambao kwa kawaida huzaliana kwa wingi na kutokuwa na faida yoyote kwa jamii, zaidi ya kuchafua mazingira na kusababisha kero kubwa kwa jamii.
Dkt. Kiwone amesema kuwa wamefanya zoezi hilo katika kitongoji cha Meriti kata ya Iliboru na kufanikiwa kufanya upasuaji wa kuhasi jumla ya mbwa dume kumi na kutoa vizazi 'ovario-hysterectomy' mbwa jike wawili.
Amefafanua kuwa zoezi hilo la kuhasi ni njia mojawapo ya kupunguza uzalianaji holela wa mbwa wasiokuwa na kazi na kupunguza tatizo la mbwa wanaozurura mitaani ambao ni kero kwa jamii.
Ameongeza kuwa mbwa wanaozurura licha ya kuwa ni kero lakini pia ni hatari sana kwa afya ya binadamu kutokana na mbwa hao kutokupatiwa chanjo wala tiba yoyote, jambo ambalo linaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa ya mbwa kwa binadamu.
Dkt. Kiwone ameelezea madhara yanayotokana na mbwa wazururaji ni pamoja maambukizi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa binadamu ugonjwa unaosababishwa na mbwa hao kutokupata chanjo ya ugonjwa huo, pamoja na uharibifu unaotokana na wizi wa mbwa unaosababisha hasara kwenye jamii.
" Mbwa anayezurura hapati chanjo wala tiba yoyote, akimng'ata mtu obvious mtu yule atapata maambukizi ya magonjwa ya mbwa huyo, pengine ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao mtu asipopata matibabu kwa haraka anaweza kupoteza maisha na matibabu yake ni ghali pia" amesema Dkt. Kiwone
John Laizer mkazi wa Ilboru amepongeza zoezi hilo kwa kuthibitisha kero ya mbwa wazururaji katika eneo lao na kusema kuwa, mbwa hao wananchafua mazingira na pia ni wezi wa vyakula na mifugo hasa kuku na mayai katika nyumba zao.
" Mbwa hawa wanatukera sana, ukisahau kidogo kufunga milango, huna bahati.., mbwa anaingia ndani na kuiba kama ni chakula, kama ni kuku kwenye banda, kiukweli wanasababishia watu hasara, tunaishi kwa hofu ya kuibiwa na mbwa, mbwa hao wamekua sio walinzi tena bali ni wezi " amesema Laizer
Hata hivyo Dkt. Kiwone amewataka wafugaji wa mbwa kuthibiti mbwa kuzaliana kwa kuwahasi na kuwatoa vizazi ili kufuga mbwa wanaoweza kumudu kuwatunza na kuepuka kero na madhara yanayoweza kuwapata binadamu kutokana na mbwa wazururaji wasiotunzwa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.