Na. Elinipa Lupembe.
Jumla ya Miradi miwili ya Elimu iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF imezinduliwa huku mradi mmoja ukitatua changamoto wa walimu kutembea umbali mrefu na kuishi ndani ya eneo la shule na mwingine ukipunguza msingamano wa wanafunzi darasani.
Miradi hiyo ni pamoja na nyumba ya walimu shule ya Msingi Laroi na vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na choo cha wanafunzi, shule ya msingi Themiyasimba kata ya Bwawani.
Miradi hiyo kwa pamoja yenye kugharimu zaidi ya shilingi milioni 130.4, imejenga nyumba ya walimu yenye sehemu mbili kwa shilingi milion 65.7 huku milioni 65.6 zikijenga vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na choo cha wanafunzi.
Mwalimu mkuu shule ya msingi Laroi mwalimu Joyce Kessy amesema kuwa uwepo wa nyumba hiyo ya walimu,licha ya kuwawezesha walimu kuishi eneo la shule lakini umewapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu hadi kufika shuleni hapo kila siku.
Ameongeza kuwa katika eneo hilo hakuna nyumba za kupangisha, jambo ambalo huwalazimu walimu waliopangiwa shuleni hapo kuishi Jiji la Arusha takribani kilomita Ishirini na hutumia usafiri wa malori ya mchanga kwenda na kurudi.
"Ukosefu wa nyumba za Walimu unawalazimu walimu kuishi mbali, wanaishi kwa Mromboo Kilomita ishirini, usafiri wa kutoka huko ni malori ya mchanga, mvua ikinyesha walimu hulazimika kusubiri mpaka mvua iishe ndipo wafike au watoke shuleni"amethibitisha mwalimu mkuu huyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mgeni rasmi na Afisa Elimu Ufundi, Sokoine Mollel, amewataka walimu na wananchi kushirikiana kwa pamoja kuitunza miundo mbinu yote iliyojengwa, kwa kuwa, kwa sasa si mali ya serikali bali ni mali ya wananchi hao.
Sokoine ameongeza kuwa, hakuna asiyefahamu adha waliyokuwa wanaipata walimu wanaofundisha shuleni hapo, jambo ambalo huwapa wakati mwingine huwapa, mgumu kuwapanga walimu katika shule hiyo.
"Walimu wanateseka kutembea, huku hakuna nyumba za kupanga, hivyo muwe na uchungu na nyumba hizi, mshirikiane kuzitunza, kuzishafisha ili zidumu kwa muda mrefu" amesisitiza Sokoine.
Hata hivyo Diwani wa kata ya Laroi, mheshimiwa Ojung Saleko, ameshauri na kuomba ramani za majengo hayo zibadilike ili ziendane na hali halisi ya uhitaji kwa kuwa nyumba hiyo ni kubwa lakini zinaishi familia mbili tu, wakati ramani ingerekebishwa ingeweza kuwa nyumba ya familia nne.
"Nitoe ushauri kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kufanya marekebisho ya Ramani za nyumba ambayo kwa gharama hiyo hiyo na ukubwa huo huo unaweza kujenga nyumba ya kuchukua familia nne na si mbili kama sasa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.