Na. Elinipa Lupembe.
Kufuatia mkakati wa serikali ya awamu ya tano, wa kupunguza na kuondoa kabisa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua nchini, halmashauri ya Arusha imefanikisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto, kwenye hospitali yake ya wilaya ya Olturumet na tayari limeanza kutumika.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, alipotembelea hospitalini hapo, kujionea hali ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, amesema kuwa, jengo hilo limesaidia kutoa huduma kwa kinamama wajawazito wa maeneo hayo, na kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kupunguza wimbi la wajawazito kujifungulia nyumbani.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa jengo hilo ambalo tayari limeweanza kutoa huduma kwa kina mama wajawazito, mradi ambao umetokana na kodi za wananchi wa halmashauri hiyo, kodi ambazo wananchi hulipa kwa halmashauri hiyo na asilimia 40 ya mapato hayo, hutumika kwenye miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo za halmashauri hiyo.
"Halmashauri imetumia shilingi milioni 130, fedha za mapato yake ya ndani, tunaendelea kujivunia uwezo wa watanzania kuanza kujitegemea kwa maendeleo yetu na kuacha kutegemea wageni, jengo zima limejengwa kwa fedha za kodi za wananchi, zinazolipwa na wananchi wa halmashauri ya Arusha, tuendee kujivunia vyetu"amesisitiza mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, wakinamama waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua, wameishukuru serikali ya awamu ya tano, imafanya mabadiliko makubwa kwa kuboresha huduma za afya hadi maeneo ya vijijini, jambo lililosababisha wao kuacha kujifungulia nyumbani na kufika hospitali ambapo kuna huduma bora.
Eva mollel (36), amethibitisha kuwa zamani walijifungulia nyumbani kwa kuwa, hosptali kulikuwa na usumbufu sana, hakukuwa na dawa, hakuna vitanda, wajawazito walilazwa wawili wawili kitanda kimoja au pengine chini, lakini kwa sasa hali imebadilika sana, kina mama wanavutiwa kuja hosptali kwa kuwa wanapata huduma bora.
Mganga mfawidhi Wodi ya Wazazi hospitali ya Olturumet Dkt. Festus Kinabo, amesema kuwa, uwepo wa jengo hilo hospitalini hapo, umeongeza idadi ya wajawazito kujifungulia hospitali tofauti na awali, jambo ambalo limesababisha kuzalisha wastani wa watoto 5 kwa siku na watoto 150 huku vifo vya mama na mtoto vikipungua kwa zaidi ya asilimia 97.
Aidha Dkt. Kinabo ameweka wazi kuwa, licha ya mafanikio makubwa ya ongezeko la wajawazito kujifungulia hospitali, bado kuna changamoto ya baadhi yao kuchelewa kufika hospitali na kujikuta wakijifungulia njiani wanapokuja hospitali, jambo ambalo bado linahatarisha maisha ya mama na mtoto.
"Niwasihi kina mama wajawazito, pindi wanapohisi au kuona viashiria vya kujifungua, wawahi hospitali ili waweze kupata huduma stahiki, kujifungulia nyumbani au njiani ni hatari sana, kunaweza kupoteza maisha ya mama au mtoto ama wote wawili"amesisitiza Dkt. Kinabo
Jengo hilo la mama na mtoto limegharimu kiadi cha shilingi milioni 130, ikiwa ni fedha za mapato ya ndani ya halmashauru ya Arusha na lilianza kujengwa rasmi mwaka wa fedha 2018/19 na kukamilika 2019/2020 na kuanza kutumika kwa wamama wajawazito.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.