Halmashauri ya Arusha imezindua siku ya upandaji miti kitaifa, huku ikiwa imejipanga kutoa miche ya miti bure kwa wananchi na taasisi ndani ya halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ilkiding'a, mgeni rasmi Afisa Utumishi halmashauri ya Arusha, Selemani Sekiete amesema kuwa, halmashauri imeandaa mkakati thabiti wa kupanda miti kwenye maeneo yote, kwa kutoa miche ya miti kwa taasisi na watu binafsi bila kulipia, kutoka kwenye kitalu cha miti cha halmashauri.
Sekiete ameongeza kuwa licha ya kutoa miche hiyo bure pia watalamu watatoa ushauri na mafunzo juu ya uoteshaji na utunzaji wa miti hiyo, sambamba na ushauri wa uoteshaji miti inayoendana na mazingira halisi ya eneo la muhitaji.
"Mwananchi anayehitaji miche ya miti, afike kwenye ofisi za halmashauri,atapatiwa miche bure pamoja na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa watalamu wetu namna ya kutunza miti hiyo" amesema Sekiete.
Aidha amefafanua kuwa kwa sasa, wananchi wanapaswa kupanda miti kama zao la biashara, zao linaloruhusu na ufugaji wa nyuki katika miti hiyo na kuwataka vijana kujikita katika upandaji wa miti katika maeneo yao.
Josephat Likindambeki mwananchi aliyeshiriki zoezi la upandaji miti, amethibitisha kupatiwa miche bure na kusema kuwa jambo hilo linawahamasisha wananchi kupanda miti na kufahamu umuhimu wa kupenda kutunza mazingira yao.
"Zamani sikufahamu umuhimu wa kupanda miti wala kutunza mazingira, nilipokwenda halmashauri kuomba miche wakanishauri na kunielekeza aina ya miti ya kuotesha na umuhimu wake kwa mazingira" amesema Likindambaki.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Afisa Wanyamapori halmashauri ya Arusha, Tabea Mollel amesema kuwa kitengo cha Maliasili kimepanga kupanda miti zaidi ya milioni 2.5 kwa mwaka huu pamoja na uhamasishaji wa ufugaji wa nyuki katika miti hiyo ili kupata malighafi za viwanda zitakazotokana mazao ya miti na nyuki.
Hata hivyo Mollel amesema kuwa licha ya jitihada za kupanda miti kwa wingi bado miti hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukame kwa baadhi ya maeneo na mifugo kwa maeneo ya wafugaji, changamoto inayopoteza zaidi ya aslimia 30% ya miti inayopandwa kila mwaka.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto hizo bado wanaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija wa kutumia eneo dogo ili kutunza mazingira yao na kuwa na mifugo michache na bora.
Awali watumishi wa halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na wananchi na wakazi wa kata ya Ilkiding'a, wamepanda jumla ya miti elfu 6, kwenye chanzo cha maji cha Saiteru katika kijiji cha Ilkiding'a katika kuazimisha siku ya upandaji miti kitaifa, yenye kauli mbiu ya 'Tanzania ya kijani inawezekana, tupande miti kwa maendeleonya viwanda'.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.