Halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na shirika lisilo la Maendeleo la SNV la nchini Uholanzi wametoa mafunzo kwa watendaji a kata 14 juu ya ujazaji wa takwimu za uwepo wa vyoo bora katika maeneo yao.
Mafunzo hayo ya siku moja yamehusisha Maafisa Watendaji wa kata 14 na maafisa watendaji wa vijiji ndani ya kata hizo, ili waweze kufuatilia takwimu za aina za vyoo, vinavyotumika kwenye kaya kwa kulinganisha na aina ya nyumba ya kaya husika.
Akizingumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa Afya halmashauri ya Arusha, Issa Msumari, amesema kuwa, watendaji wa kata na vijiji wanatakiwa kupita nyumba kwa nyumba, kufanya ukaguzi wa vyoo vinavyotumika kwenye kaya na kutambua aina ya vyoo kwa kulinganisha na nyumba inayotumika.
Ameongeza kuwa, takwimu hizo zitasaidia kutambua hali halisi ya matumizi ya vyoo bora katika maeneno hayo, kufuatia mafunzo ya uhamasishaji ya ujenzi wa vyoo bora yaliyotolewa kwenye kaya hizo kufuatia kampeni ya nyumba ni choo.
"Imeonekana kuwa, kaya inajenga nyumba bora ya kuishi na kusahau ujenzi wa choo bora, bila kufahamu kuwa nyumba ni choo, unakuta nyumba nzuri but choo cha ovyo,hakina hata usiri, kimezungushiwa maturubai". amesema Msumari
Hata hivyo Afisa Afya huyo, amefafanua kuwa, takwimu zinaonesha kuwa asilimia 3 ya wakazi wa halmashauri ya Arusha hawana vyoo bora na kuongeza kuwa kupitia kampeni ya nyumba ni choo, halmashauri inategemea kufikia aslimia 100 ya matumizi ya vyoo bora mwishoni mwa mwaka huu.
Mshauri wa masula ya Usafi na Mazingira wa shirika la SNV, Anna Emmanuel, amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watendaji wanakusanya takwimu sahihi za matumizi ya vyoo, kwenye kaya katika maeneo yao.
Takwimu hizi zitatoa taswira ya hali halisi ya matumizi ya vyoo, ambazo zitawezesha kupata hali halisi ya mabadiliko ya tabia ya jamii kutoka kwenye tabia ya kunya nje na kwenda kunya chooni, kwa kuwa tendo hilo ni la siri na linahitaji choo bora.
Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha Oljoro, Lootha Sikoreim amethibitisha kuwa, watu wengi katika maeneo ya vijijini, wanapojenga nyumba, choo huwa hakipo kwenye bajeti, mara nyingi hujenga kwa hutumia vifaa vilivyobaki baada ya ujenzi wa nyumba kukamilika.
"Ni kawaida mtu anajenga nyumba, baada ya nyumba kukamilika anatumia vipande vya tofali, mabaki ya mabati, saruji kujenga choo, kwa hali hiyo lazima choo hakitalingana na nyumba, na wakati mwingine pesa ikiisha basi choo hakitajengwa" amesema Sikorei
Hata hivyo elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi, ili kuhakikisha ujenzi wa nyumba unaendana na ujenzi wa vyoo ili kuwe na uwiano kati ya nyumba na choo.
Maafisa Watendaji waliopata mafunzo hayo ni wa kata za Nduruma, Lemanyata, Bwawani, Musa, Laroi, Oldonyosambu,Kisongo, Oldonyowas, Tarakwa, Sambasha, Oljoro, Kiutu na Olturoto.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.