Maafisa Eimu kata wa Halmashauri ya Arusha, wliaya ya Arumeru, wametakiwa kubuni mbinu za usimamizi wa shule wanazozisimamia ili kuboresha njia za ufundishaji kwa walimu, kwa lengo la kupandisha taaluma katika shule na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba katika halmashauri hiyo.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Msingi, Halmashauri ya Arusha, mwalimu Hossen Mghewa, wakati akizungumza na Maafisa Elimu hao wa ngazi ya kata, katika kikao kazi cha siku moja, chenye lengo la kukumbushana utekelezaji wa majukumu ya kazi, pamoja na kubadilishana uzoefu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kikao kilichofanyika ndani ya ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mghewa amewasisitiza maafisa Elimu hao, kusiwamamia walimu katika maeneo yao na kuhakikisha shughuli za ufundishaji zinafanyika kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha walimu hao, wanatumia maarifa katika kubuni na kutengeneza zana za kufundishia kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira yao, pamoja na kutumia zana hizo wakati wa kufundisha, mbinu ambazo zitakazorahisisha tendo zima la ufundishaji kwa wanafunzi.
Mghewa amewataka Maafisa hao, kwenda kukaa na walimu kwenye shule zao, kuweka mikakati thabiti ya kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia zana rahisi na kuwajengea uwezo wanafunzi wa madarasa ya mitihani mbinu sahihi za kujibu mitihani, ili kufuta alama D na F kwenye matokeo ya mitihani yao, huku akisisitiza kuwa jambo hilo linawezekana endapo walimu watajituma na kufanya kazi yao kwa bidii na maarifa.
Aidha amewataka Maafisa hao, kufanya ukaguzi mara kwa mara shuleni, ili kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili walimu na wanafunzi katika shule hizo na kuhakikisha tendo la kufundisha na kujifunza linafanyika kwa ufanisi na kwa kufuata misingi na taratibu zote za ufundishaji, huku akisisitiza kusimamia maadili na nidhamu kwa walimu pamoja na kuthibiti utoro kwa waalimu na wanafunzi.
"Msikae ofisini, zungukeni kwenye shule zenu, ili kukagua ufundishaji wa walimu katika maeneo yenu, kagueni kazi za walimu na wanafunzi, kagueni mahudhurio ya walimu na kuhakikisha ufundishaji unafuata misingi na taratibu, hii itawasaidia kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati" amesisitiza Mghewa.
Hata hivyo, amewataka kuwakutanisha walimu wa masomo na kujadiliana na kupeana uzoefu wa mbinu bora za ufundishaji, jambo litakalowawezesha kujengeana uwezo kati ya walimu wenyewe na kujenga mazingira rafiki ya ufundishaji, kwa lengo la kukuza ufahamu wa KK tatu za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi ili pasiwepo mwanafunzi anayeshindwa kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha Mghewa ameagiza kuwepo na daftari malumu kwa kila shule, daftari la kutunza kumbukumbu za utendaji kazi ili kurahisha upatikanaji wa taarifa hizo muhimu, pindi zinapohitajika pamoja na kuhamasisha utendaji kazi kwa waalimu.
"Ninaagiza kuwepo kwa daftari maalumu kwa kila shule, kwaajili ya kutunza kumbukumbu za utendaji kazi wa walimu, naamini taarifa hizo zitaongeza ari kwa waalimu katika kufanya kazi kwa bidii na kuwabaini wale wote wanaofanya kazi kinyume na maadili" amesema Afisa elimu huyo.
Hata hivyo Maafisa Elimu hao, wameridhishwa kikao kazi hicho na kuthibitisha kuwa, kukutana kwao kumewawezesha kupata maarifa mapya kwa njia ya kujadiliana kwa pamoja changamoto, zinazoikabili sekta ya elimu, pamoja na kubadilishana uzoefu miongoni mwao, huku wakisisitiza kutumia maarifa na maelekezo yaliyotolewa, katika kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kupandisha kiwango cha taaluma.
Mwenyekiti wa Maafisa Elimu hao wa kata na Afisa Elimu wa kata ya Oljoro, mwalimu Furahini Godson, amesema kuwa, kikao kazi hicho kimewajenga upya na kuahidi kwenda kutumia maarifa hayo kwenye vituo vya vya kazi huku akiahidi kutekeleza maagizo yote pamoja na kutoa ushirikiano ilikufikia malengo ya halmashauri ya kufuta F na D kwa shule za msingi.
"Binafsi ninashukuru uwepo wa kikao hiki, licha ya kubadilishana uzoefu, kimkao kimetukumbushana utekelezaji wa majukumu yetu ya kazi, naahidi kwenda kuyafanyia kazi maagizo yote kwa kushirikiana na walimu katika shule zangu na wadau wengine wa elimu" amesema mwalimu Godson.
Kikao kazi hicho kimewakutanisha maafisa Elimu kutoka kata 27 za halmashauri ya wilaya ya Arusha, wanaosimamia jumla ya shule 141 za msingi za halmashauri hiyo.
Afisa Elimu Msingi, Halmashauri ya Arusha, Mwwlimu Hossein Mghewa akizungumza na Maafisa Elimu ngazi ya Kata, wakati wa kikao kazi cha siku moja, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.