Na. Elinipa Lupembe.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule leo amewaongoza watumishi wa makao makuu ya halmashauri hiyo, kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya halmashauri, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano, la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mtambule, amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira yao, kwa kufanya usafi katika maeneo yote yanayowazunguka pamoja na kuhakikisha taka zote, zinahifadhiwa katika vyombo na maeneo sahihi, maeneo ambayo hayaruhusu takataka hizo kusambaa na kusababisha uchafu tena, mara baada ya kusafisha.
Aidha amewasisitiza wananchi, kusimamia usafi kwenye maeneo ya umma kama mitaro na barabara, ili watu wenye nia mbaya wasitupe takataka na kuchafua maeneo yetu na kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake ili kuwabaini watu wanaotupa takataka kwenye maeneo hayo.
"Niwatake wananchi kusimamia usafi kwenye maeneo yetu, tuwabaini wote wanaotupa takataka kwenye mitaro na barabara, ili usafi tunaoufanya uwe na maana kwa afya na maisha yetu sote" amesisitiza Mkurugenzi huyo
Hata hivyo watumishi na wananchi walioshiriki kufanya usafi huo, wamefurahishwa na zoezi hilo na kuahidi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao kila wakati huku wakihakikisha utunzaji wa taka na kulinda maeneo ya mitaro na barabara zote.
Fidelis Lukumai, mkazi wa Ngaramtoni licha ya kufurahishwa na zoezi hilo, lililofanya pamoja na mkurugenzi wa halmashauri yao, wamesema kuwa usafi ni muhimu kwa kila mtu, na kuahidi kuendeleoa kusafisha mazingira yao pamoja na kuwabaini wanaotupa takataka katika mitaro na barabara zinazozunguka kwenye maeneo yao.
Awali Mkurugenzi Mtambule, watumishi pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo, wa halmashauri ya Arusha, walianza kufanya usafi mapema saa 12:00 asubuhi, na kufanikiwa kufanya usafi katika hospitali ya wilaya ya Olturumet, eneo la Ngaramtoni, Oliorieni eneo la kwa Idd pamoja na eneo la soko la Kisongo na viunga vyake, huku wananchi na wakazi wa maeneo hayo wakijitokeza kwa wingi kuungana na watumishi, kuusafisha maeneo yanayowazunguka.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.