Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu mpya wa wilaya ya Arumeru, mheshimiwa Jerry Muro leo amepata fursa, ya kukutana na kuzungumza na watumishi wa halmashauri ya Arusha kwa mara ya kwanza, moja kati ya halmashauri mbili za wilaya hiyo ya arumeru, mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya, amekutana na watumishi wa halmashauri hiyo, wakati akitambulishwa kwao, na mkuu wa wilaya ya Monduli mheshimiwa Idd Kimanta, aliyekuwa akikaimu ukuu wa wilaya ya Arumeru, kwa takribani miezi nane sasa.
Mheshimiwa Muro baada ya kutambulishwa, amewataka watumishi wa halmashauri ya Arusha, kufanyakazi kwa bidii na uadili mkubwa, huku wakifuata kanuni na madili ya kazi na kuwasisitiza kuwa wanyenyekevu na wakarimu katika kuwahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa, anafahamu mheshimiwa Rais John Pombe Mgufuli, anahitaji kuwahudumia wananchi wanyonge, hivyo watumishi wote wa serikali ni lazima watoe huduma bora kwa kuwajali sana wananchi na si kutoa huduma kwa ubabaishaji.
"Ninachowaka watumishi wa Arusha DC, tucheze ngoma ya pamoja, ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ngoma yenye lengo la kuwahudumia wananchi walio wanyonge, kwa kuwajali wananchi wote, kama yalivyo matakwa ya mheshimiwa Rais wetu" amesema mkuu huyo wa wilaya
Aidha amewaonya, wale wanaodhani kuwa kasi ya rais Magufuli, ni nguvu ya soda wanajidanganya, huku akifafanua kuwa anachokitamka na anachofanya, mheshimiwa Rais, anamaanisha na hana utani na watumishi waonaokwenda kinyume na taratibu za nchi hii.
"Narudia kusema tena na tena, jamanii asiyetaka kuendana na kasi ya Rais Magufuli na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, atupishe, na ikiwezekana tupishane mapema pale tuu, ninapoingia ofisini" amesisitiza mkuu huyo wa wilaya
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida kwa watumishi hao, mheshimiwa Muro amemuagiza Afisa Maendeleo ya Jamii, halmashauri ya Arusha, kuandaa andiko la kuanzisha SACCOS ya wafanyakazi, ili kuwawezasha watumishi hao, kuweka na kukopa.
Ameahidi kuhakikisha SACCOS hiyo inasimamiwa vizuri, huku akisisitiza kuwa hawezi kufanyakazi na watumishi wasio na fedha na wenye njaa kali, jambo linalowasababisha kupokea rushwa na kufanya ubadhilivu kwenye fedha za Umma.
Mtumishi mwenye njaa, ni rahisi kushawishika, kuomba na kupokea rushwa pamoja na kutamani fedha za miradi na kuwasisitiza watumishi hao, kujipanga kuanzisha SACCOS, itakayowezesha wafanyakazi wote kujiinua kiuchumi.
Naye mkuu wa wilaya ya Monduli, baada ya kumtambulisha mkuu huyo mpya wa wilaya ya Arumeru, alitamka kumkabidhi watumishi wa Arusha DC wakiwa weupe, wenye afya njema, wanyenyekevu na wachapakazi na kuwataka watumishi hao, kumpa ushirikiano mkuu huyo wa wilaya kama ilivyokuwa kwake, kwa kipindi kifupi alichofanya katika halmashauri ya Arusha.
Nao Watumishi wa halmashauri ya Arusha, wamempongeza mkuu wa wilaya ya Arumeru kwa kuaminiwa na kuteluliwa kwake, na kuahidi kushirikiana nae kufanyakazi kwa weledi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya chama cha Mapinduzi, kwa kasi ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tuu.
Awali mkuu wa wilaya ya Arumeru mheshimiwa Jerry Muro, ameanza kazi rasmi leo ya kuwatumikia wanaArumeru, mara baada ya kuapishwa jana na mkuu wa mkoa wa Arusha, mheshimiwa Mrisho Gambo mara baada ya kuteuliwa na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.