Halmashauri ya wilaya wa Arusha imepokea jumla ya pikipiki 18 kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za elimu kwa ngazi ya kata, pikipiki ambazo zitatumiwa na Maafisa Elimu ngazi ya kata, kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za elimu kwenye shule wanazozisimamia ndani ya kata zao.
Akizungumza mara baada ya kupokea pikipiki hizo Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera amesema kuwa, pikipiki hizo zitakuwa chachu ya uwajibikaji hasa katika kurahisisha utendaji kazi kwa maafisa elimu wa ngazi ya kata.
Ameongeza kuwa kulingana ya Jiografia ya halmashauri ya Arusha, hasa kwa kata za pembezoni, kuna umbali mkubwa kutoka shule moja na nyingine, jambo lililokuwa linawawia vigumu maafisa elimu hao, kuratibu shughuli zao kwa ufanisi.
Hata hivyo amethibitisha kuwa, kutokana na uwepo wa vitendea kazi hivyo, anaamini sekta ya elimu kuendelea kuboreka zaidi kwa kuwa na usimamizi mzuri katika ukusanyaji wa taarifa pamoja na ukaguzi wa utendaji kazi wa walimu na shule kwa ujumla.
" Kwa kuwa sasa maafisa elimu wamepata usafiri, naamini watakwenda kusimamia vizuri utendaji kazi wa walimu shule, ukusanyaji wa takwimu na usimamizi wa shule kwa ujumla wake huku tukitegemea kupandisha taaluma pamoja na kuongeza ufaulu" amesema Mkurugenzi Mahera.
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari, halmashauri ya Arusha, Charles John amesema kuwa,, pikipiki hizo zitakwenda kutatua changamoto nyingi shuleni, kutokana na ugumu uliokuwepo kwa baadhi ya maeneo, wa kuzifikia shule kwa wakati.
"Kulikuwa na ugumu kwa Afisa Elimu kata kutembelea kwa mguu kukagua shughuli za utendaji shuleni kutoka na umbali mrefu wa kutoka shule moja mpaka nyingine, lakini kupatikana kwa usafiri huu kutarahisha kuzifikia shule na kuwa na usimamizi thabiti" amesema Afisa Elimu huyo.
Januari Ambros, mkazi wa Sakina ameipongeza serikali ya awamu ya tano, kwa kuona umuhimu wa kutoa vitendea kazi kwa ajili ya kurahisisha usimamizi na ukaguzi wa kazi zinazofanywa ma walimu na wanafunzi shuleni.
Licha ya pongezi hizo Ambros, ameiomba serikali, kuangalia namna ya kuwapanga wanafunzi wanaokwenda sekondari kwenye shule za jirani au kujenga mabweni ili kuondoa changamoto kubwa wanayoipata watoto njiani wakati wa kwenda na kurudi nyumbani.
"Watoto wanajikuta wamejiingiza kwenye vitendo vibaya ikiwemo mimba na uvutaji wa bangi, wanapokutana na watu wasio wema njiani na kujikuta wanashawishika kuingia kwenye mitego ambayo mwisho huwa na madhara makubwa kwa wanafunzi hao" amesema Ambrosi.
Serikali ya awamu ya tano, inaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kutatua changamoto za elimu ikiwemo kutoa elimu bila malipo, miradi ya ujenzi wa miundo mbinu ya shule kupitia miradi ya P4R pamoja na kuanza kutoa vyombo vya usafiri kwa Maafisa Elimu kata kwenye halmashauri nchini.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.