Halmashauri ya Arusha kupitia Idara ya Mifugo imejipanga kuboresha uzalishaji wa ng'ombe bora wa maziwa kwa kutoa mafunzo kwa wafugaji ndani ya halmashauri.
Mikakati hiyo inafuatia teknolojia ya uhamilishaji safu za koo za ng'ombe wa maziwa 'artificial insemination', zoezi lililoanza kufanyika mapema mwaka uliopita, 2017.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Daktari wa Mifugo, halmashauri ya Arusha Dkt. Yohana Kiwone amesema kuwa, lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwafanya wafugaji kuhama kutoka ufugaji wa mazoea usio na faida na kuanza ufugaji wa kisasa unaowapeleka wafugaji, kwenye uzalishaji wa kibiashara.
Dkt. Kiwone ameelezea umuhimu wa uhamilishaji ni koboresha safu za koo za ng'ombe, kwa kumpandikiza ng'ombe mbegu bora yenye nyama na maziwa mengi kwa kufuga ng'ombe wachache kwenye eneo dogo.
Ameongeza kuwa, licha ya telnolojia ya uhimilishaji kuimarisha ufugaji kwa kuwa na ng'ombe bora, teknolojia hii inakwenda sambamba na utunzaji wa mazingira.
Aidha Dkt Kiwone amethibitisha kuwa, kupitia mafunzo hayo mfugaji anajengewa uwezo wa kufahamu vizuri mbegu na koo ya ng'ombe anayemfuga pamoja na kuwa na kumbukumbu, zenye taarifa sahihi za ng'ombe wake.
"Wafugaji wengi wanafuga ng'ombe bila hata kufahamu aina wala ukoo wa ng'ombe anayemfuga, wala kuwa na taarifa na kumbukumbu sahihi za ng'ombe wake jambo lililokuwa linawafanya wafugaji kufuga kwa mazooea na kuendelea kuwa masikini" amesema Daktari huyo.
Hata hivyo, Wafugaji wamefurahia mafunzo hayo, kwa kusema kuwa wameanza kupata mwanga wa mafanikio kupitia mifugo ambayo awali, wamekua wakifuga kwa mazoea bila kuwa na utalamu wowote.
Wafugaji hao wamekiri mifugo yao inawapa chakula tuu na si zaidi ya hapo licha ya gharama kubwa wanazotumia kuhudumia ng'ombe hao.
Naishiye Laizer mkazi wa Losikito amethibitisha kuwa, wafugaji wengi katika maeneo yao hupata kiasi kidogo cha maziwa kinachotumika kwa familia na kuuza kiasi kidogo sana.
" Mifugo yetu inatupatia maziwa ya kunywa watoto nyumbani, kama ni kuuza tunauza maziwa kidogo lita moja au mbili,wakati tunatumia nguvu nyingi na uzalishaji ni mdogo kabisa" amesema Naishiye.
Hata hivyo Naishiye amekiri kuwa, mafunzo hayo yamewafungua macho na kuwapa mwanga wa matunda bora, yanayoweza kupatikana kupitia ufugaji bora hasa kupitia utalamu wa uhamilishaji.
Awali Dkt. Kiwone amefafanua kuwa halmashauri imepanga kutoa mafunzo kwa wafugaji 900 kwa awamu ya ya kwanza mpaka kufikia mwezi Agosti mwaka 2018 na mpaka jumla ya wafugaji 427 wameshafikiwa ndani ya vijiji na vitongoji vya Mamlaka ya mji mdogo Ngaramtoni.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.