Na. Elinipa Lupembe.
Wauguzi halmashauri ya Arusha, wametakiwa kuacha tabia ya kufanya kazi ya uuguzi kama biashara, na badala yake kufanyakazi hiyo kwa weledi, kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo ya uuguzi, huku wakiongozwa na imani, heshima, upendo, upole, unyenyekevu na uvumilivu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Utumishi, halmashauri ya Arusha, Juma Mpume wakati akifungua kikao kazi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kilichowakutanisha wauguzi wanaotoa huduma kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi ndani ya halmashauri ya Arusha, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mpume amefafanua kuwa, taaluma ya uuguzi ni taaluma nyeti, ambayo inagusa uhai wa binadamu, hivyo inahitaji unyenyekevu, upendo na kuwataka wauguzi hao kuwa na imani pindi wanapowahudumia wagonjwa, na kujikita kutoa huduma kwa weledi na kufuata miongozo inayoongoza taaluma ya uuguzi kwa wagonjwa.
Amefafanua kuwa, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na wauguzi, bado kuna malalamiko mengi kutoka kwa wagonjwa, juu ya rushwa na lugha chafu, iwe hospitali za Serikali hata zile za binafsi, tabia ambayo ni kinyume cha maadili ya utumishi wa Umma na maadili ya Uuguzi pia.
Aidha Mpume, amewaonya baadhi ya wauguzi wasio waaminifu, wanaochafua taaluma hiyo, kwa kudai rushwa na kutoa lugha mbaya kwa wagonjwa, kuacha mara moja tabia hiyo, tabia ambayo licha ya kuwaathiri wagonjwa kisaikolojia, inachafua weledi wa taaluma ya Uuguzi kwa ujumla wake.
"Kazi yenu inagusa maisha ya binadamu, haihitaji mzaha wala vipingamizi, wahurumieni wagonjwa, kuweni makini kuokoa maisha yao, wale wanaotaka chochote kabla ya kutoa huduma waache tabia hiyo, tambueni kufanya hivyo kuna madhara makubwa kwa wagonjwa na jamii kwa ujumla wake " Amesema Mpume.
Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Dkt. Wedson Sichalwe, alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na wauguzi hao, kutokana na kuhamia kufanyakazi kwenye mkoa wa Arusha, na kuanza kwa kuwapongeza wauguzi hao, kwa kufanya kazi kwa bidii licha ya changamoto ndogo zinatokana na baadhi ya wauguzi wasio waaminifu.
Mganga mkuu huyo, amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imetoa kipaumbele kikubwa kwenye Sekta ya Afya, kwa kuboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa lengo la kuhakikisha, watoa huduma za afya wanafanya kazi kwenye mazingira rafiki yatakayowezesha, mwananchi kupata huduma bora kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya hadi hospitali.
Ili kufikia lengo la Serikali la kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi na kupunguza vifo vya mama na mtoto, Wauguzi ndio kiungo cha kufikia malengo hayo, kwa kuhakikisha kila mtu anayefika kwenye kituo cha afya anapata huduma bora na stahiki.
Aidha Dkt. Sichalwe, amewashauri kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa maji na umeme, kwenye vituo vyao vya afya kupitia bajeti zao za vituoni, huduma ambayo ni muhimu sana kwenye vituo vya afya.
Hata hivyo wauguzi hao, wamekiri bado kuwepo na wauguzi wachache, wanaoichafua taaluma hiyo kwa kudai rushwa na kutumia lugha ambayo si rafiki kwa wagonjwa, na kuahidi kuendelea kurekebishana na kuonyana kama binadamu, huku wakiahidi kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia kanuni na taratibu za utoaji wa huduma kwa wateja wao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi mkoa wa Arusha (TANNA) na muuguzi, Sista Gladness Mtui ameshukuru uwepo wa kikao kazi hicho ambacho kimetumika kuwanoa upya na kuwakumbusha wauguzi maadili ya kazi zao, na kuahidi kuendelea kusimamia maadili ya taaluma yao, nyeti ya uuguzi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.