Katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, Halmashauri ya Arusha imehuisha SACCOS ya vijana 'ARUSHA DC VIJANA SACCOS, kwa lengo la kuhamasisha na kuwajengea uwezo vijana wa kuweka na kukopa.
SACCOS hiyo iliyokuwa imepoteza mwelekeo na kuwa kama imekufa kwa kipindi kirefu, imeweza kuhuishwa na kuanza upya kwa kuwakutanisha vijana wenye lengo la kuwa wajasiriamali, kwa ajili ya kuunganisha nguvu pamoja, kwa kuanza kununua hisa, kukopeshana wao kwa wao pamoja na nakukopesha vikundi vingine ili kuinuana kiuchumi.
Wakizungumza wakati wa mkutano mkuu wa kwanza wa SACCOS hiyo, kwenye ofisi ya vijana halmashauri, wanaSACCOS hao wamesema kuwa, wanatambua umuhimu wa kuunganisha nguvu ili kujengeana uwezo wa kupata mihitaji na kuanzishia biashara kuelekea uchumi wa viwanda.
Nsesheye Nkota amethibitisha kuwa, SACCOS hiyo itarudisha matamani ya vijana wasio na ajira katika halmashauri ya Arusha na kuwapa fursa ya kupata mitaji, itakayowawezesha kujiajiri na kuondokana na changamoto ya vijana wengi kuwa uzururaji kwa kukosa ajira.
"SACCOS hii imeleta matumaini kwetu vijana, kutokana na wengi wetu, kukosa ajira na kushindwa kujiajiri kutokana na kukosa mitaji, hali inayosababusha vijana wengi kuwa wazururaji" amesema Nkota.
Aidha katika mkutano huo wa kwanza, umefanyika uchaguzi wa viongozi, na kumchagua, Evaline Zakayo kuwa mwenyekiti, makamu mwenyekiti ni Mihayo Zakaria na Hamidu Abubakary katibu ili kuiongoza SACCOS hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza Mara baada kushinda nafasi ya mwenyekiti, licha ya kuwashukuru wajumbe kwa kumchagua, Evaline ameahidi kufanya kazi kwa bidii, ili kufikia malengo ya SACCOS hiyo na kutimiza ndoto za vijana kuelekea uchumi wa viwanda.
Evaline amesema hii ni fursa nzuri kwakwe, ya kuhamasisha vijana wenzake, kutumia fursa za kilimo na mifugo, zinazopatikana kwenye maeneo wanayoishi kwa kuziongezea thamani na kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini linalowakabili vijana wengi.
"Natambua dhamana niliyopewa , naamini kupitia nafasi hii nitapata fursa ya kukutana na vijana wengi, kazi yangu kubwa ni kuwahamasisha kubuni biashara zinazotokana na kilimo na ufugaji, kwa kutumia mitaji midogo kuongeza thamani mazao hayo na kuanzisha viwanda vidogo.
Ameongeza kuwa, ukosefu wa ajira kwa vijana, umesababisha vijana wengi kukata tamaa na wengine kujikuta wakijiingiza kwenye vitendo viovu na kuwataka vijana kupambana ili kukabiliana hali ngumu ya maisha, bila kukata tamaa.
Sambamba na hayo ameitaka serikali kupita halmashauri zake nchini kuwejengea uwezo vijana wa kujitegemea pamoja na kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, kuweka na kukopo ili kuwasaidia kutambua njia sahihi za matumizi ya mikopo inayotolewa na serikali.
Kwa upande wake Afisa vijana, Halmashauri ya Arusha, Ahadi Mlai amesema malengo ya SACCOS hiyo ni kuwasaidia vijana kuweka akiba na kutumia akiba hizo kukopa, ili kuwainua kiuchumi na kuongeza wigo mpana wa kubuni na kutekeleza fursa za ajira zinazowazunguka.
Aidha, amewataka viongozi waliochaguliwa kuwa wabunifu, waaminifu na waadilifu katika kusimamia na kutekeleza majukumu ili kufikia malengo ya SACCOS hiyo.
ARUSHA DC VIJANA SACCOS imeanza na wanachama vijana 34, na inasimamiwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana kwa kushirikuana na Kitengo cha Ushirika, na kuhakikisha SACCOS hiyo inazaa matunda na vijana hao kufikia malengo.
Mwenyekiti wa ARUSHA DC VIJANA SACCOS, Evaline Zakayo
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.