Watu wengi wamekua na tabia ambazo ni kinyume na maadili, tabia ambazo hata mzazi anashangaa mtoto wake amezipata wapi, lakini kwa asilimia 80, tabia ya mtoto inajengwa na mzazi na mlezi kuanzia mimba mpaka umri wa miaka mitatu.
Kutokana na uelewa mdogo wa wazazi na kushindwa kupembua mambo chanya ya kumjengea mtoto katika umri huo,husababisha mtoto kushindwa kujitawala na kutawala mazingira yanayomzunguka kiakili, kimwili, kihisia na kisaikolojia.
Tafiti zinaonyesha kuwa elimu duni ya wazazi na walezi juu ya malezi na makuzi ya mtoto husababisha udumavu kwa watoto kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Tabia anazokuwa nazo mtu mzima, ziwe mbaya au nzuri ni matokeo yaliyojengeka kwa mtoto kuanzia kipindi cha mimba mpaka alipofikisha umri wa miaka mitatu.
Ubongo wa mtoto, unategemea zaidi kupewa/ kujazwa vitu kutoka kwa wazazi na walezi pamoja na watu wanaomzunguka kuanzia kipindi cha mimba mpaka miaka mitatu ili uweze kukua na kumjenga mtoto huyu uwezo wa utambuzi.
Hayo yamethibitishwa na Afisa Ustawi wa Jamii, halmashauri ya Arusha, Beatrice Tengi, wakati akitoa mafunzo kwa wauguzi wa afya wa kitengo cha huduma za mama na mtoto wa halmashauri ya Arusha na Jiji la Arusha, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa SEDHA Jijini Arusha.
Afisa Ustawi huyo na mwezeshaji wa mafunzo hayo amesema kuwa, wauguzi waliopata mafunzo hayo, wanakwenda kutoa mafunzo juu ya vichocheo changamshi muhimu kwenye makuzi ya mtoto kwa wazazi na walezi kila wanapofika Kliniki kuanzia wakati wa kliniki ya mama mjauzito na mara baada ya mtoto kuzaliwa mpaka miaka mitano.
Aidha Afisa Usatawi huyo amesema kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kuelewa umuhimu wa kufahamu mambo yakuzingatia katika hatua za malezi na makuzi ya mtoto, kuanzia mimba mpaka miaka mitatu ndio yanayojenga mtoto kuwa na tabia nzuri au mbaya.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha mimba mpaka miaka mitatu,mtoto anatakiwa kupewa elimu changamshi yenye vichocheo chanya, itakayoanza kumjengea uwezo mtoto wa kukua kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Kwa mtoto mpaka kufikia umri wa miaka mitatu, ubongo wa mtoto unakuwa tayari umejaa kwa asilimia 80, asilima 20 iliyobaki, huongezeka kwa kipindi kilichosalia cha maisha yake yote.
Hivyo katika umri huu ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha wanamjenga na kumjaza mtoto maadili mema yatatayomfanya mtoto kuwa na mitazamo chanya itakayomuwezesha kufanikiwa katika maisha yake ya baadae.
Vichocheo chanya kutoka kwa wazazi na walezi na vinamfanya mtoto aweze kujitambua, kujiamini, kujifunza zaidi na uwezo wa kupembua mema na mabaya, hivyo wazazi na walezi wana jukumu kubwa sana la malezi ya mtoto mpaka atakapofikisha umri wa miaka mitatu" amesema Tengi.
Endapo mtoto atakosa vichocheo chanya ni dhahiri mtoto huyu atakua hajiamini, uwezo mdogo wa kujifunza, hawezi kujitegemea, muoga na mwenye wasiwasi na kuwa na mahusiano mabaya na jamii katika maisha yake.
Tengi ameongeza kuwa kipindi chote cha ujauzito mtoto anatakiwa kujazwa mambo mema ikiwemo upenda na kujaliwa na baada ya kuzaliwa mpaka miaka mitatu mtoto anapaswa kufundishwa mambo chanya ya kijamii.
Hata hivyo Tengi amethibitisha kuwa makosa yanayofanywa na wazazi na walezi kwenye hatua za malezi na makuzi ya mtoto yanamadhara makubwa sana kwa maisha ya mtoto hasa anapokuwa mtu mzima.
Amewataka wazazi na walezi kushirikiana katika hatua zote za makuzi ya mtoto kwa kumchochea vichangamshi chanya na kuongeza kuwa wazazi ni lazima kuzungumza na mtoto mambo mema, kuacha kutukana, kumsemea mtoto mambaya badala yake kumuonyesha upendo zaidi, kumjali na kumfanya ajitambue,ajiamini, ajithamini na kuthamini wengine kuanzia anapozaliwa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.