Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Pastori Mnyeti amewapa siku tatu wakazi wa kitongoji cha Ilkiurei kata ya Kiranyi waliojenga nyumba kwenye mkondo wa maji kubomoa wenyewe nyumba hizo kabla serikali haijaanza kubomoa kutokana na nyumba hizo kuzuia maji kupita na kusababisha maji kujaa ndani ya nyumba nyingi za wakazi hao hasa wale wasio na uwezo wa kujizatiti kwa maji hayo pindi mvua zinaponyesha.
Mhe. Mnyeti amezungumza hayo wakati alipotembelea maeneo ya Kitongoji hicho na kushuhudia uharibifu mkubwa unaotokana na maji hayo kukosa mwelekeo na kuishia kwenye nyumba za watu na kuhatarisha maisha ya watu hao.
Mkuu huyo wa wilaya amemuagiza mhandisi wa barabara halmashauri ya Arusha Mhandi Fredi Mboye na viongozi wa kata na kitongoji hicho akiwemo Diwani wa kata ya Kiranyi Mhe. Jombi Seneu kukaa kikao cha kupanga mkakati wa utekelezaji wa kubomoa nyumba hizo kama wananchi hao watakaidi amri ya kubomoa kwa hiari yao wenyewe.
Awali Mhe. Mnyeti alitembelea eneo hilo baada ya mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Fatiki Kingazi mkazi wa Unga Ltd Jijini Arusha kufariki dunia kutokana na nyumba aliyokuwa amelala kujaa maji na ukuta kuanguka katika eneo la Mangurueni kitongoji cha Ilkiurei kata hiyo ya Kiranyi.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 09.04.2017 lililosababishwa na maji ya mvua iliyokuwa ikinyesha kujaa kwenye nyumba hiyo na kusababisha ukuta wa nyumba hiyo kuanguka kutokana na maji hayo kukosa mwelekeo kwa kuwa wakazi wa maeneo hayo wamezuia mkondo huo wa maji kwa kujenga.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.